Boda boda, bajaji sasa kulipa kodi kila mwaka

Ofisa Mkuu wa Usimamizi wa Kodi TRA, Hamadi Mterry akitoa elimu ya mabadiliko ya sheria ya fedha  ya mwaka 2023 kwa walipakodi wa wilaya ya Bariadi (hawapo pichani). Picha na Samirah Yusuph.

Muktasari:

Pikipiki za biashara zinazobeba abiria zitachangia kodi ya Sh65,000 kila mwaka huku, pikipiki za miguu mitatu maarufu kama bajaji zitaichangia kodi ya Sh120,000.

Bariadi. Wafanyabiashara ya usafirishaji wa abiria kwa pikipiki za miguu miwili maarufu kama bodaboda wataanza kulipia Sh65,000 kama kodi kwa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA).

Kodi hiyo ni miongoni mwa mabadiliko ya sheria ya fedha ya mwaka 2023 iliyopitishwa kwenye bunge la bajeti la mwaka 2023/2024 inayojumuisha sheria 15 zilizofanyiwa marekebisho.

Akitoa elimu ya mabadiliko ya sheria ya kodi ya mwaka 2023 Agosti 11, 2023 mjini Bariadi, Ofisa Mkuu wa Usimamizi wa Kodi TRA, Hamadi Mterry amewataka kujivunia kuchangia  Serikali.

“Pikipiki za biashara zinazobeba abiria wataichangia serikali yao pendwa Sh65,000 kwa mwaka, pikipiki za miguu mitatu maarufu kama bajaji tunawapigia magoti waichangie Serikali yao pendwa Sh120,000 kwa mwaka na wajivune kwa hilo," amesema Mterry

Sambamba na hilo kodi zilizoondolewa ni pamoja na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) katika bidhaa zinazozalishwa kutoka katika zao la pamba ili kuongeza tija ya kilimo na kuwanufaisha wakulima.

"kuondolewa kwa kodi itasaidia kuzalisha kwa wingi bidhaa zinazotokana na pamba mfano tulikuwa na uhaba wa vitenge katika nchi hali iliyosababisha vitenge vikaanza kuingizwa kwa njia isiyo sahihi, Serikali imeondoa ushuru kwenye bidhaa hizo zinazozalishwa na pamba ili kuweza kumrahisishia mkulima kuzalisha pamba kwa wingi na pamba hizi zitakazozalishwa ziweze kutengeneza bidhaa nyingi,” amesema Benjamin John, Ofisa Elimu na Mawasiliano kwa Umma TRA mkoani Simiyu.

Kodi nyingine iliyoongezeka ni kodi ya majengo ambayo imekuwa ikilipwa kupitia makato katika huduma ya kununua umeme kutoka Sh1, 000 kwa mwezi hadi Sh1,500.

Baadhi ya walipa kodi wamesema kodi hiyo bado inamkanganyiko kwa wateja wenye mita zaidi ya moja.

“TRA wanatuelekeza kuandika barua tanesco lakini zinapofika huko hazijibiwi kwahiyo changamoto hiyo ingepatiwa ufumbuzi mapema,"amesema Phillips Mtiba mfanyabiashara wilayani Bariadi.