Bodaboda watatu kunyongwa kwa kumuua abiria kwa nondo

Muktasari:

Siku ya mauaji hayo Mei 21, 2020, washitakiwa walikuwa baa, mshitakiwa wa kwanza, Yohana Mwambejele, alimuona Geofrey Manionga (marehemu) akiwa na begi akiingia baa

Mbeya. Maandiko ya dini yanasema, “anayeua kwa upanga naye atakufa kwa upanga,” ndivyo unaweza kuelezea hukumu ya madereva watatu wa pikipiki za kukodi (bodaboda), waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kumuua abiria wao.

Tukio hilo lilitokea Mei 21, 2020 eneo la St Aggrey Wilaya ya Uyole mkoani Mbeya, bodaboda hao walikula njama na mmoja wao akamshawishi marehemu apande pikipiki yake ili njiani washirikiane kumpora begi waliloshuku lilikuwa na pesa.

Hukumu hiyo imetolewa Machi 4, 2024 na Jaji Emmanuel Kawishe wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya baada ya kuwatia hatiani bodaboda hao kwa kosa la kumuua Geofrey Manionga kwa kumpiga kwa nondo kichwani na kusababisha fuvu kupasuka.

Waliohukumiwa kunyong’wa hadi kufa ni Yohana Mwambeleje aliyekuwa mshitakiwa namba moja ambaye simu ya marehemu aliyoiiba na kuiuza ndio iliyowakamatisha wenzake ambao ni Andrea John na Rogers Mwakingile.

Jaji Kawishe amesema ushahidi wa upande wa mashitaka umethibitisha shitaka hilo pasipo kuacha shaka kwamba, washitakiwa ndio waliomuua marehemu huku  wakikiri kutenda unyama huo walipohojiwa polisi na kupelekwa eneo walilofanya mauaji.

Licha ya maelezo yao hayo, lakini Jaji amesema upo ushahidi wa mawasiliano ya simu ya Mtandao wa Halotel ambao ndio ulisaidia kuunganisha matukio na kufanikiwa kukamatwa kwa washitakiwa na simu na taarifa vilitolewa kama kielelezo mahakamani.

“Ukichukua ushahidi wa upande wa mashitaka kwa jumla wake, ninashawishika kuwa mnyororo wa matukio uliunganika na haukuvunjika. Kwa mazingira hayo naona upande wa mashitaka umeweza kuthibitisha kuwa ni washitakiwa walimuua Geofrey,”amesema Jaji Kawishe.

“Ushahidi unaonyesha lengo lao lilikuwa ni kumpora fedha marehemu. Kwa kuwa walipanga kabla na kutekeleza kosa, nia ovu imeweza kuthibitishwa na upande wa mashitaka kutokana na ushahidi wa mashahidi na kukiri kosa kwa washitakiwa.

“Kwa hiyo nawatia hatiani washitakiwa kwa kosa la mauaji. Katika sheria ya makosa ya jinai, kuna adhabu moja tu kwa kosa la kuua kwa makusudi nayo ni kunyongwa hadi kufa. Kwa hiyo nawahukumu washitakiwa kunyongwa hadi kufa,”amesisitiza Jaji Kawishe.

Mauaji yalivyofanyika

Siku ya mauaji hayo Mei 21,2020, washitakiwa walikuwa baa, mshitakiwa wa kwanza, Yohana Mwambejele, alimuona marehemu akiwa na begi akiingia baa akionekana mlevi ndipo mshitakiwa huyo alijifanya kuzungumza naye.

Hapo ndipo, mshitakiwa huyo aliposhuku marehemu ana pesa, hivyo aliwafuata mshitakiwa wa pili, Andrea John na wa tatu, Rogers Mwakingili na kuwashirikisha na kuwaeleza marehemu atakapokuwa anatoka, atamshawishi apande pikipiki yake.

Mshitakiwa huyo alisema watakapokuwa wanaondoka na marehemu eneo hilo, mshitakiwa wa pili na wa tatu  wamfuate ili waweze kumpora fedha alizokuwa nazo kwenye begi alilobeba.

Baada ya muda fulani kupita, marehemu alitoka; mshitakiwa wa kwanza aliwatonya wenzao kuwa mlengwa anatoka.

Mshitakiwa alienda kusimama karibu na mlango na kufanikiwa kumshawishi Manionga (marehemu) apande pikipiki yake.

Mshitakiwa wa pili na wa tatu waliwafuata kwa nyuma na walipofika eneo la St Aggrey, mshitakiwa huyo wa kwanza alisimamisha pikipiki na kutoa Nondo iliyokuwa imefichwa kwenye pikipiki na na kumpiga nayo marehemu kichwani na akaanguka chini.

Hapo ndipo mshitakiwa wa pili na wa tatu walipopekua mifuko ya nguo za marehemu na kumkuta akiwa na simu aina ya Itel na akatokea rafiki yao mwingine anayejulikana kwa jina la King ambaye alichukua begi lililoaminika kuwa na pesa na kuondoka nalo.

Walichokisema mashahidi

Shahidi wa kwanza, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Joram Rwezimila amesema wao walikuwa wanachunguza mauaji hayo na makachero wawili, Ajini Exahaud na Koplo Msamaha walikuwa na nambari za utambulisho (IMEI), za simu ya marehemu iliyoporwa.

Walituma barua kwenda kampuni za simu ili kupata taarifa za nani alikuwa anatumia simu hiyo, na ndipo kampuni ya Halotel iliwajibu Septemba 8,2020 hiyo ikiwa imeshapita miezi minne, kuwa simu hiyo sasa iko hewani kwa maana inatumika.

Kwa kutumia taarifa hizo, waliweza kumkamata mtu aliyekuwa akitumia simu hiyo, Emmanuel Ambokile ambaye alinunua na katika mnyororo huo ndio wakamfikia mshitakiwa wa kwanza aliyewaongoza kuwapata mshitakiwa wa pili na wa tatu.

Shahidi wa pili, Emmanuel Ambokile katika ushahidi wake alielezea namna alivyonunua simu hiyo na kuelezea namna alivyoshirikiana na polisi hadi kumpata mshitakiwa wa kwanza, akiwa Polisi alishuhudia washitakiwa hao wakikiri kufanya mauaji.

Kwa upande wake, shahidi wa tatu, Rebeca Manionga ambaye ni dada wa marehemu, alieleza kuwa Septemba 15,2020 alipokea simu kutoka kituo cha kati cha polisi, wakimtaka aende kutambua vitu vya marehemu na aliweza kutambua simu yake.

Shahidi wa nne ambaye ni askari polisi F.4948 Sajini Msamaha alieleza namna alivyoandika maelezo ya onyo ya mshitakiwa wa kwanza na alikiri kutekeleza mauaji hayo na kwamba mipango ilianzia katika baa ya King Leaders iliyopo Uyole.

Frank Daudi aliyekuwa shahidi wa tano, yeye ni mwenyekiti wa waendesha bodaboda ambaye aliitwa polisi ili ashuhudie kile ambacho bodaboda wawili walikuwa wakikieleza, aliwasikia wakizungumzia kupora na suala la mauaji alilisikia alipofika St Aggrey.

Shahidi wa sita, Exhaud Mundeme alieleza namna alivyopewa jukumu la kuandika maelezo ya Elizabeth Manionga ambaye ni mama wa marehemu alielezea namna mwanaye alivyotoweka ghafla na baadaye mwili wake kuokotwa eneo la St Aggrey.

Pia, alielezea namna simu ya marehemu ilivyofuatiliwa na kubainikwa ikitumiwa na mtu mwingine na namna walivyomkamata na kueleza kuwa bila simu ya marehemu pengine wasingeweza kupata mwanga wa kuwanasa washitakiwa.

Shahidi wa saba, Mrakibu wa Polisi (SP) alisema Mei 29,2020, mama wa marehemu alikwenda ofisini kwake akilalamika kuwa kifo cha mwanaye hakikuwa kimesababishwa na ajali ya barabarani na vitu vyote alivyokuwa navyo havikupatikana.

Hapo ndipo uchunguzi ulipoanza, walifuatilia mawasiliano ya simu ya marehemu na kufanikiwa kumpata mtu aliyekuwa akiitumia ambaye naye alisema alikuwa ameinunua kwa mtu mwingine ambaye naye alikuwa ameinunua kwa Yohana.

Polisi walifanikiwa kuwakamata washitakiwa na katika mahojiano, shahidi huyo alisema walikiri kufanya mauaji na waliwapeleka polisi hadi eneo walipofanya mauaji.

Daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu, Dk William Mulla ambaye alikuwa shahidi wa nane, alisema alibaini sababu ya kifo ni jeraha lilikuwa sehemu ya kichwani na alikuwa anatoa damu puani na kwamba fuvu la kichwa nalo lilikuwa limevunjika.


Walivyojitetea kortini

Katika utetezi wake, mshitakiwa wa kwanza, Yohana Mwambenjele ameelezea namna alivyokamatwa na polisi Septemba 22,2020 na Oktoba 1,2020 alichukuliwa na kupelekwa chumba cha upelelezi na kupewa karatasi asaini bila kujua nini kimeandikwa.

Hata hivyo, amesema alikataa kusaini hadi afahamu inahusu nini ndipo mpelelezi akamweleza kuwa anakabiliwa na shitaka la mauaji, alikataa kusaini na aliteswa kwa kipigo ndio maana alikubali kusaini karatasi hizo na kuweka dole gumba.

Mshitakiwa wa pili, Andrea John alijitetea kuwa yeye alikamatwa Septeba 14,2020 na aliwekwa mahabusu hadi Septemba 22 alipotolewa na kupelekwa chumba cha upelelezi na mpelelezi akamtaka akubali chochote atakachokuwa anaulizwa.

Kama ilivyokuwa kwa mshitakiwa wa kwanza, naye alisema aliteswa kwa kipigo na kukubali kila alichoelezwa na alifungwa kitambaa usoni na kupakiwa kwenye gari na wakaondoka na gari liliposimama na kushushwa aligundua ni St Aggrey.

Mshitakiwa huyo alisema waliamua kukubali kuwa walimpora mtu eneo hilo kwa sababu ya kuhifia bunduki walizokuwa nazo polisi na kwamba hicho kinachosemwa kuwa alikiri kwa hiyari yake kushiriki tukio hilo si cha kweli kwani ni baada ya kuteswa.

Mshitakiwa wa tatu, Rodgers Mwakingili alisema Septemba 14,2020 akiwa na vijana wenzake sita wakicheza kamari eneo la Shule ya Msingi Asanga walifika polisi saa 5:00 usiku na kuwakamata, kuwapiga na kuwapakiza ndani ya gari lao.

Alidai walipofikishwa polisi, mmoja wa polisi wa upelelezi alimfunga pingu na kumning’iniza juu ya dari na kupigwa na kwamba siku moja saa 8 mchana alifungwa kitambaa usoni na kutolewa mahabusu na aliposhushwa kwenye gari alijikuta St Aggrey.

Alieleza kuwa siku ya tukio hilo hakuwepo Uyole bali alikuwa Songwe Viwandani na kueleza kuwa ushahidi wa upande wa mashitaka unaonyesha alikamatwa Septemba 13,2020 baada ya kutajwa na Yohana na sio kwamba alishiriki tukio hilo.