Bodi ya mikopo yatoa orodha ya wanufaika wengine 698
Muktasari:
Leo Jumamosi, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) nchini Tanzania imetoa majina 698 walioshinda rufaa zao hivyo kupangiwa mikopo.
Dar es Salaam. Wanafunzi 698 washinda rufaa na kupangiwa mikopo yenye thamani ya Sh2.46 bilioni.
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) nchini Tanzania imetangaza orodha ya majina hayo leo Jumamosi Desemba 7, 2019 ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliofanikiwa kupata mikopo katika dirisha la rufaa kufuatia kukosa au kupata kiwango kidogo cha mkopo katika awamu nne zilizopita.
Wanafunzi hao 698 wamepangiwa mikopo yenye thamani ya Sh2.46 bilioni hivyo kufanya jumla ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliopata mikopo hadi sasa kufikia 49,485.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru amesema taarifa zaidi kuhusu viwango walivyopangiwa zinapatikana katika akaunti zao binafsi walizotumia kuomba mkopo – Student’s Individual Permanent Account (SIPA) kupitia https://olas.heslb.go.tz
“Tumeshaweka taarifa za hawa wanafunzi katika mfumo na hivyo kila mmoja anatakiwa aingie katika akaunti yake ya SIPA ambapo ataona taarifa zake ambazo pia zinatumwa vyuoni,” amesema Badru.
Kwa mujibu wa Badru, HESLB imeboresha mifumo yake hivyo wanafunzi wote wa mwaka wa kwanza walioomba mikopo wanaweza kuona taarifa zao kutoka popote walipo kwa kutumia simu zenye mtandao wa intaneti (simu janja).
“Taarifa ya kina kuhusu utoaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2019/2020 itatolewa wiki ijayo baada ya uchambuzi wa mwisho kukamilika, ”amesema Badru.