Bomoabomoa mpya kutikisa Dar

Bomoabomoa mpya kutikisa Dar

Muktasari:

  • Baadhi ya wakazi wa Kimara watakumbana na bomoabomoa nyingine baada ya Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) mkoa wa Dar es Salaam kutoa notisi ya siku 30 ya kuondoa nyumba, kuta, uzio au fremu za biashara zilizo katika hifadhi ya barabara ya Morogoro.

Dar es Salaam. Baadhi ya wakazi wa Kimara watakumbana na bomoabomoa nyingine baada ya Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) mkoa wa Dar es Salaam kutoa notisi ya siku 30 ya kuondoa nyumba, kuta, uzio au fremu za biashara zilizo katika hifadhi ya barabara ya Morogoro.

Kwa mujibu wa barua iliyosainiwa na kuthibitishwa na Kaimu Meneja wa Tanroads mkoa wa Dar es Salaam, Eliamin Tenga, Tanroads inatarajia kuanza kuboresha eneo hilo hivi karibuni ili kuondoa changamoto ya foleni katika eneo hilo.

Katika barua hiyo ya Julai 9 iliyoelekezwa kwa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kimara, Tanroads inaeleza kwamba maboresho hayo yamekusudiwa kutokana na kuongezeka kwa magari ambayo yanasababisha msongamano kuanzia Kimara Korogwe hadi Ubungo.

“Tunapenda kukutaarifu kuwa Serikali kupitia Tanroads mkoa wa Dar es Salaam, imetenga fedha kwa ajili ya kutatua changamoto za msongamano wa magari eneo la Kimara Bucha hadi Kimara Resort katika barabara ya Morogoro,” inaeleza taarifa hiyo.

Barua hiyo inaeleza kwamba hifadhi ya barabara ya Morogoro ina upana wa mita 90 kutoka katikati ya barabara kila upande kuanzia Ubungo hadi Kimara Stopover.

Tenga alieleza katika barua hiyo kwamba tangu mwaka 1997, 2014 na 2017, ofisi ya meneja wa Tanroads mkoa wa Dar es Salaam ilitoa notisi za kuondoa majengo, kuta na vibanda vya biashara katika eneo hilo la hifadhi ya barabara.

Alisema ujenzi wowote uliofanyika katika hifadhi ya barabara ni kinyume na Sheria ya Barabara, kanuni za hifadhi ya barabara na ilani ya Serikali namba 161.

“Tanroads mkoa wa Dar es Salaam inakukumbusha kuondoa nyumba, kuta, uzio au fremu na vibanda vya biashara vilivyomo kuanzia eneo la Kimara Bucha mpaka Kimara Resort ndani ya hifadhi ya barabara katika muda wa siku 30 kuanzia tarehe ya notisi hii,” inaeleza barua hiyo.

Alipoulizwa kuhusu bomoabomoa hiyo, mkuu wa wilaya ya Ubungo, Kheri James alisema hana taarifa hizo kutoka Tanroads na akizipata atatoa mtazamo wa Serikali ya wilaya.

“Taarifa hiyo haijafika ofisi kwangu, nikiipata nitatoa mtazamo wa Serikali ya wilaya, lakini kwa sasa sijapokea taarifa hiyo na hawawezi kuongea na wananchi mpaka taratibu hizo zipite katika ofisi yangu,” alisema James.

Hii si mara ya kwanza kufanyika kwa operesheni ya kubomoa nyumba zilizo katika hifadhi ya barabara eneo la Kimara. Mara ya mwisho bomoabomoa ilifanyika mwaka 2017, huku wananchi kadhaa wakipoteza makazi yao.

Operesheni hiyo iliyoanza mwishoni wa Julai 2017, ilihusisha takriban nyumba 1,300 zenye thamani na matumizi tofauti ambazo kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na wamiliki, wengi wao walidai ziliwagharimu kati ya Sh40 milioni hadi zaidi ya Sh1.3 bilioni hadi kukamilisha ujenzi wake bila kuhusisha bei ya kiwanja.

Bomoabomoa hiyo ilisababisha maumivu kwa wananchi wengi kwa sababu walipoteza makazi yao, bila kulipwa fidia yoyote kwa kile kilichoelezwa na Serikali kwamba walijenga ndani ya hifadhi ya barabara.

Baada ya bomoabomoa hiyo, Serikali ilianza upanuzi wa barabara ya Morogoro yenye njia nane kuanzia Kimara hadi Kibaha na hadi sasa ujenzi wa barabara hiyo unakaribia kukamilika, huku ikitarajiwa kutatua changamoto ya foleni.

Mbali na wananchi kupoteza makazi yao, Shirika la Umeme nchini (Tanesco) nalo lililazimika kuvunja sehemu ya jengo lake lililopo Ubungo baada ya kubainika kwamba lilikuwa ndani ya hifadhi hiyo ya barabara.