Bosi mpya wa Magereza kuanza na mambo sita

Kamishna Mkuu wa Magereza, Mzee Ramadhan Nyamka (kushoto) akikabidhiwa kikombe kutoka kwa mtangulizi wake, Meja Jenerali Suleiman Mzee. Picha na mpiga picha wetu
Muktasari:
- Kamishna Mkuu mpya wa Jeshi la Magereza, Mzee Ramadhan Nyamka ametaja vipaumbele atakavyovitekeleza, ikiwamo kuweka misingi mizuri ya kuwapokea na kuwahifadhi wananchi wanaopokelewa magerezani.
Dar es Salaam. Kamishna Mkuu mpya wa Jeshi la Magereza, Mzee Ramadhan Nyamka ametaja vipaumbele atakavyovitekeleza, ikiwamo kuweka misingi mizuri ya kuwapokea na kuwahifadhi wananchi wanaopokelewa magerezani.
Nyamka (58), ametaja vipaumbele hivyo ikiwa ni siku moja tangu Rais Samia Suluhu Hassan, amteue kushika wadhifa huo.
Awali bosi huyo wa magereza alikuwa Kaimu Kamishna wa Magereza, upande wa huduma na urekebu na amekipokea kijiti kutoka kwa Meja Jenerali Suleiman Mzee ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Vipaumbele vyake
Vipaumbele vingine alivyovibainisha jana alipozungumza na gazeti hili ni kuimarisha nidhamu, kufanya kazi kwa weledi, kujenga umoja na mshikamano kwa kuwafanya watumishi kuzungumza lugha moja.
Pia aliahidi kuendelea kuboresha programu za kurekebisha wafungwa, ili wakitoka, jamii iwaone wamebadilika na mwisho kubeba mazuri yaliyoachwa na mtangulizi wake.
“Rais ameonyesha imani kubwa kwangu kwa kuniteua kuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, lakini imani hii napaswa kuilipa na najiona nina deni kubwa na namna bora ya kulipa ni kufanya kazi kwa weledi,” alisema.
Kuhusu wananchi wanaopelekwa magerezani, alisema jeshi litatoa msukumo mkubwa katika jukumu la kuwalinda na kurekebisha tabia za wananchi waliovunja sheria, ili kuona wanabadilika na wawe tayari kujiunga na wenzao katika ujenzi wa shughuli za kimaendeleo wanapomaliza vifungo.
“Tuko kwenye mchakato wa kufanya mabadiliko ya programu za urekebishaji, ili kuona tunafanikiwa katika dhana nzima ya urekebishaji wa wahalifu wanaoletwa magerezani,” alisema.
Akiwa mwenye furaha wakati wote wa mazungumzo kwa njia ya simu, Nyamka alisema peke yake hawezi kulifanya jeshi hilo kuwa bora, bali atahakikisha anashirikiana na wenzake kwa kuzingatia weledi katika utendaji kazi wa kila siku na kuacha tabia za kujenga makundi au kunyoosheana vidole.
Aidha, alikumbushia ziara ya Rais Samia ya Machi 25 mwaka huu alipotembelea makao makuu ya jeshi hilo kuzindua na kuweka mawe ya msingi kwa baadhi ya miradi, akiasa kuwa jeshi hilo ni mali ya Watanzania isipokuwa viongozi wamepewa dhamana ya kuliongoza.
“Kwa kauli ile nina jukumu kubwa la kulisimamia jeshi hili kwa niaba ya Watanzania na kufanya yale yote yanayotarajiwa kufanyika, ikiwamo kujenga nidhamu ndani ya jeshi na jeshi lolote haliwezi kufanikiwa bila nidhamu, nitahakikisha inakuwepo,” alisema.
Nyamka anakuwa Kamishna Mkuu wa 16 wa Jeshi la Magereza, huku wa kwanza akiwa Mwingereza, Patrick Manley aliyeongoza kuanzia mwaka 1955 hadi 1962 na kufuatiwa na wengine wazawa waliochukua nafasi baada ya uhuru.
Wakati Nyamka akieleza vipaumbele hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni akiwasilisha bajeti ya wizara kwa mwaka 2022/23, bungeni jijini Dodoma alizungumzia hali ya ulinzi na usalama magerezani.
Alisema hadi Machi mwaka huu jumla ya wafungwa na mahabusu 32,671 walikuwepo katika magereza yote nchini, sawa na asilimia 9.2 zaidi ya uwezo wa magereza wa kuwahifadhi wafungwa na mahabusu 29,902.
Masauni alisema kati ya wafungwa hao, 16,883 wamehukumiwa kutumikia adhabu mbalimbali gerezani na 15,788 ni mahabusu ambao wanaendelea kusikiliza kesi zao mahakamani.
Alisema katika jitihada za kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani, Serikali inatumia utaratibu wa kifungo cha nje (EML), parole, huduma kwa jamii na huduma za uangalizi kutoa wafungwa wenye viashiria vya kurekebishika tabia.
Wadau wampa neno
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alisema anategemea haki jinai kwa wafungwa zinapewa nafasi kubwa huku akieleza taasisi yake imekuwa ikitembelea magereza mbalimbali na kubaini changamoto ya wafungwa kutopata haki zao.
“Wakifungwa hawawezi kukata rufaa kwa sababu kuna makosa yanayokatiwa rufaa. Kwa mfano, aliyeua bila kukusudia. Tukiwa Morogoro tulikuta wafungwa wametoka kanda ya ziwa wamepelekwa pale kufanya shughuli za kilimo, wakati kesi zao hazijaisha,” alisema.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa aliyesema wanataka kuona maboresho katika chombo hicho, kwa kuwa ni eneo linaloshughulikia watu, hivyo misingi ya haki za binadamu inapaswa kuzingatiwa.
Kwa upande wake, Dk Paul Loisulie kutoka Chuo Kikuu Dodoma (Udom), alisema: “Wanatakiwa kuzalisha chakula kwa wingi na kuacha kutegemea ruzuku kutoka serikalini, lakini wafungwa hao wanaweza kutumika kufanya kazi nyingine, ili chombo hicho kiweze kujiongezea mapato yake na kujiendesha.”