Bosi wa zamani Rivacu mikononi mwa Takukuru

Bosi wa zamani Rivacu mikononi mwa Takukuru

Muktasari:

  • Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Manyara inamshikilia aliyekuwa mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika cha bonde la ufa (Rivacu), Lohay Langai kwa tuhuma za kutoa ajira bila idhini ya bodi ya chama hicho.

Babati. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Manyara inamshikilia aliyekuwa mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika cha bonde la ufa (Rivacu), Lohay Langai kwa tuhuma za kutoa ajira bila idhini ya bodi ya chama hicho.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Manyara, Holle Makungu ameyasema hayo mjini Babati leo Alhamisi Januari 14, 2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Makungu amesema Langay anatuhumiwa kufanya kosa hilo Novemba mosi, 2017 akiwa mwenyekiti wa Rivacu.

Amebainisha kuwa alitumia vibaya nafasi yake kwa kuingia mkataba wa ajira ya uhasibu na Paul Makoye bila idhini ya bodi ya wakurugenzi wa chama hicho cha ushirika.

Amesema katika uchunguzi wamebaini katika mkataba huo,  Makoye aliingia mkataba bila idhini ya bodi ya wakurugenzi wa chama hicho cha ushirika na kujipatia ujira wa Sh2.6 milioni.

"Kitendo cha kuajiri bila kibali ni kosa la matumizi mabaya ya ofisi kinyume na kifungu cha 31 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007," amesema Makungu.

Amesema Langay anatarajiwa kufikishwa  mahakama ya hakimu mkazi wa Mkoa wa Manyara na kusomewa shtaka hilo na mwendesha mashtaka wa Takukuru,  Martin Makani.