Bosi ZMA aipa neno Serikali

Muktasari:

  • Serikali imeombwa kuridhia mikataba ya kimataifa ya kuhifadhi mazingira ya usafiri wa bahari kwa kusimamia ulinzi wa sekta hiyo pamoja na kuendesha vyombo kwa usalama.

Kilwa. Serikali imeombwa kuridhia mikataba ya kimataifa ya kuhifadhi mazingira ya usafiri wa bahari kwa kusimamia ulinzi wa sekta hiyo pamoja na kuendesha vyombo kwa usalama.

Ombi hilo limetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Bahari Zanzibar (ZMA), Sheikha Akhmed alipokuwa akizungumza katika hafla ya kufunga maadhimisho ya siku ya usafiri wa maji duniani ambayo kitaifa yamefanyika wilayani Kilwa mkoani Lindi.

Mikataba hiyo iliyowekwa na na Shirika la Kimataifa la kusimamia bahari (IMO), ni pamoja na wa kuzuia umwagwaji wa maji ya ballast yatokayo katika meli, kuzuia uchafuzi wa mazingira utokanao na meli pamoja na Annex VI inayohusu uharibifu wa hali yahewa na sheria ya kupunguza sulphur kwenye meli ijulikanayo kama IMO sulphur 2020.

"Tunapozungumzia usafirishaji wa kijani tunalenga usafirishaji wa mizigo na watu baharini kwa kutumia rasilimali chache kadri inavyowezekana ili kulinda mazingira yasiathiriwe na uchafuzi utakanao na mafita yanayotumiwa na vyombo vya habari.

"Usafirishaji wenye kulinda mazingira unahamasisha nchi wanachama kujenga tamaduni za kutunza mazingira na kusimamia uendeshaji wa bandari na vyombo vya baharini ili kuhakikisha vinafuata sheria za usalama zilizowekwa kitaifa na kimataifa," amesema.

Naye Mkuu wa Wilaya hiyo, Zainab Kawawa amewataka wakazi wa wilaya hiyo kuzingatia mafunzo waliyopewa kuhusu utanzaji wa bahari na mazingira yake ili kusaidia kukuza uchumi.