BoT kupokea sarafu zisizotumika

Muktasari:

  • Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza kuanza kupokea sarafu za Sh200, 100 na 50 ambazo hazitumiki na kuzibadilisha na noti.

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza kuanza kupokea sarafu zilizotunzwa kwa muda mrefu na kuzibadilisha na noti.

 Hatua hiyo inatokana na mamlaka iliyonayo BoT katika usimamizi wa sarafu kupitia Sheria ya mwaka 2006 inayotoa mamlaka kwa benki hiyo pekee kutengeneza na kutoa fedha (noti na sarafu) kwa matumizi nchini Tanzania.

Taarifa iliyotolewa jana Ijumaa, Desemba 29, 2023 na Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba imeeleza huduma ya kupokea sarafu zilizotunzwa kwa muda mrefu bila kutumika itatolewa kwa wananchi wote au taasisi ili kubadilishwa na noti.

Amesema huduma hiyo itatolewa katika ofisi zote za BoT na benki za biashara nchini.

"Hatua hii imechukuliwa kutokana na utafiti uliobaini kuwepo kwa sarafu nyingi za Sh200, 100 na 50 ambazo hazitumiki kwa muda mrefu katika mzunguko wa kiuchumi na badala yake zimetunzwa au kuwekwa nyumbani, ofisini, kwenye magari, biashara na taasisi mbalimbali nchini," amesema Tutuba.

Amesema huduma hiyo itatolewa kama kazi maalumu ya mwezi mmoja kuanzia Januari 2, 2024 ili kuendelea kulinda ubora wa sarafu dhidi ya uharibifu unaotokea katika mazingira yasiyokuwa salama na kurejesha fedha hizo kwenye mzunguko wa kiuchumi.

"Wananchi wote wenye sarafu za Sh00, 100 na 50 ambazo zimetunzwa bila kutumika kwa muda mrefu na wangependa kuzibadilisha ili kupata noti au kuzitunza kama amana katika akaunti zao, wanaombwa kuziwasilisha kwenye ofisi za Benki Kuu au benki za biashara kwa ajili ya kupata huduma hiyo," amesema Tutuba.