BOT yapigilia msumari matumizi ya fedha za kigeni nchini

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imepigilia msumari katazo lake la matumizi ya fedha za kigeni kwa wakazi wa Tanzania katika kulipia bidhaa na huduma nchini.

Msisitizo huo umetolewa baada ya tamko la kwanza kutolewa Agosti 2007 na la pili Desemba 2017.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Gavana wa BOT, Emmanuel Tutuba inaeleza kuwa katika siku za karibuni imebainika kuwepo kwa ukiukwaji wa tamko hilo na kueleza kuwa maagizo yaliyotolewa hapo awali kuhusu matumizi ya fedha za kigeni yanapaswa kuendelea kuzingatiwa.

Imeeleza kuwa bei za bidhaa na huduma zote hapa nchini zitangazwe kwa shilingi ya Tanzania ikijumuisha kodi za kupangisha ardhi, nyumba na ofisi, gharama za elimu, huduma za afya, vifaa tiba na vitendanishi, usafiri, lojistiki na bandari, vifaa vya kielektroniki na huduma za mitandao ya mawasiliano na nyinginezo.

Pia bei ambazo walengwa wake wakuu ni watalii au wateja wasio wakazi zinaweza kutangazwa kwa fedha za kigeni na malipo yake yanaweza kufanyika kwa fedha za kigeni, zinajumuisha gharama za hoteli, usafiri, gharama za viwanja vya ndege na viza kwa wageni, usafirishaji kwenda nchi za nje kupitia Tanzania na gharama za mizigo bandarini.

"Walipaji wanaotumia fedha za kigeni watambuliwe kwa vitambulisho vyao kama pasi za kusafiria na nyaraka za usajili kwa makampuni," amesema gavana huyo katika taarifa hoyo na kuongeza;

"Mkazi yeyote wa Tanzania anapaswa kufanya malipo kwa kutumia shilingi yaTanzania pekee na hivyo asilazimishwe kulipia bidhaa au huduma yoyote hapa nchini kwa kutumia fedha za kigeni."

Vilevile taarifa imeeleza kuwa kifungu cha 26 cha Sheria ya BOT mwaka 2006 kinaelekeza kuwa shilingi ya Tanzania ndiyo fedha pekee ambayo inaruhusiwa kutumika nchini, hivyo hakuna mtu au kampuni yoyote inayoruhusiwa kuikataa kwa malipo yoyote halali hivyo kwenda kinyume ni kuvunja sheria hiyo.