Brela yaeleza kuridhishwa urasimishaji biashara Nanenane

Msaidizi wa huduma kwa wateja kutoka wakala wa usajili biashara na leseni (Brela) Amour Mwalanga (kulia) akikabidhi cheti mfanyabiashara Aza Nsilia baada ya kurasimisha biashara yake.

Muktasari:

Maonesho ya wakulima Nanenane yaliyodumu kwa siku nane, ambapo yalifunguliwa na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, Agosti 1, na kufungwa na Rais Samia Sulu Hassan, Agosti 8 jijini Mbeya.

Mbeya. Siku tatu baada ya kumalizika kwa sherehe za maonesho ya wakulima Nanenane, wakala wa usajili wa biashara na leseni (Brela) imeelezea mafanikio makubwa waliyopata kwa kipindi hicho.

Maonesho ya wakulima Nanenane yalifanyika kitaifa katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya na kushirikisha viongozi wa serikali akiwamo Rais Samia Suluhu Hassan aliyefunga kilele cha sherehe hizo, Agosti 8.

Akizungumza leo Alhamisi Agosti 11, Mkuu wa kitengo cha uhusiano Wakala wa usajili wa biashara na leseni (Brela), Royda Andusamile amesema wamejivunia mwitikio wa wafanyabiashara katika kurasimisha biashara zao.

Alisema kwa kipindi cha siku nane walizohudumu kwenye maonesho hayo, zaidi ya wafanyabiashara 200 walirasimisha biashara zao, jambo ambalo kwao ni mafanikio makubwa.

“Lengo letu ilikuwa kutoa elimu ya urasimishaji biashara na hadi tunamaliza Nanenane tumerasimisha watu 262, zoezi hili ni endelevu nchi nzima kwa sababu faida ya urasimishaji inamsaidia mfanyabiashara kupata mikopo,” amesema Royda.


Kwa upande wake Gwamaka Mwakenja mtaalamu wa Tehama amesema changamoto kubwa kwa wateja wao imekuwa ni kushindwa kutumia kujaza taarifa zao mtandaoni, jambo ambalo wamekuwa makini kulifanyia kazi.

“Kama ni tatizo la intaneti tumekuwa tukitoa usaidizi kupitia mawasiliano ya moja kwa moja kumuelekeza mteja namna ya kufanya na tumeweza kufanikisha kwa kiasi kikubwa,” amesema Mwakenja.

Naye Aza Nsilia kutoka kampuni ya Nsansa Farm inayojishughulisha na ufugaji na uuzaji maziwa, amesema ameamua kurasmisha biashara yake ili kuwa huru na shughuli hiyo.

“Inamaana hata nikifanikiwa siiku za usoni nitakuwa huru kufanya shughuli zangu kwakuwa nitakuwa najulikana na nimepewa cheti rasmi,” amesema Aza.