Bunge kujadili umri wa mgombea urais Kenya

Muktasari:

Spika Justin Muturi amesema ameiamuru Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Sheria (JLAC) kuchambua ombi hilo na kuwasilisha ripoti bungeni baada ya siku 60.

Nairobi, Kenya. Bunge la Kenya limesema litashughulikia pendekezo la kuzuia mtu yeyote mwenye umri wa miaka 70 na zaidi kuwania urais na nyadhifa nyingine za kisiasa nchini humo.

Spika Justin Muturi amesema ameiamuru Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Sheria (JLAC) kuchambua ombi hilo na kuwasilisha ripoti bungeni baada ya siku 60.

Ombi hilo liliwasilishwa na Mohamed Mohamud, mkazi wa Garissa ambaye anataka Bunge liifanyie mabadiliko Katiba ili kudhibiti umri wa wagombea mbalimbali wa nyadhifa za kisiasa.

Kwa mujibu wa Mohamud, siyo haki kwa watumishi wa umma kushinikizwa kustaafu wanapofikisha umri fulani, ikiwa wanasiasa wanaotaka kuwania nyadhifa katika chaguzi hawajadhibitiwa kiumri.

Amesema  mwenendo huu unawafanya viongozi wakongwe kukataa kuondoka katika ulingo wa siasa, "ili kutoa nafasi kwa kizazi cha wanasiasa wenye umri mdogo."
Mohamud  amesema  mtu mwenye umri wa miaka 70 hawezi kutekeleza  majukumu ya uongozi ipasavyo.

Hata hivyo, wabunge wa Jubilee na Nasa walipuuza pendekezo hilo wakisema kulishughulikia ni sawa na kulipotezea Bunge muda wake.
Baadhi yao wamesema  pendekezo hilo ni sehemu ya mkakati wa kumzuia kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2022.
Mbunge Robert Pukose alisema ombi hilo litaharibu mandhari ya siasa nchini hasa baada ya Odinga kuamua kushirikiana na Rais Uhuru Kenyatta.
"Pendekezo hili linapoteza muda  wa bunge na halingekubaliwa. Lina malengo mabaya na linafaa kukataliwa. Tunapaswa kuunda sheria kwa manufaa ya vizazi vijavyo hatutakiwi kuunda sheria zinazolenga watu fulani," alisema Dk Pukose ambaye ni mbunge wa Jubilee.
Naye Mbunge wa Mvita, Abdulswamad Nassir alisema pendekezo hilo linafaa kupewa muda mchache zaidi kwa sababu "halina maana yoyote."
"Mtu akiwasilisha ombi kama hili bunge, kamati husika inafaa kulipa muda wa dakika tatu pekee. Hii itazuia watu wengine kuwasilisha maombi mengine yasiyo na maana bungeni," amesema Nassir ambaye ni mbunge wa ODM.

Kiongozi wa wengi bungeni, Aden Duale hata hivyo amesema kila Mkenya ana haki ya kuwasilisha ombi bungeni kuhusu suala lolote kama kipengele cha 118 cha Katiba kinavyopendekeza.

"Huenda ombi hili sio nzuri. Huenda halina mwelekeo lakini hatutakiwi kupuuza kwani wananchi wengine wataogopa kuwasilisha maombi bungeni siku nyingine,"

amesema Duale ambaye ni mbunge wa Garrisa Mjini.

Ametoa wito kwa kamati ya JLAC inayoongozwa na Mbunge wa Baringo Kaskazini, William Cheptumo kuandaa ripoti ambayo itatoa mwelekeo kuhusu maombi kama hayo siku zijazo.

Licha ya kusema kuwa anashukuru malengo ya ombi hilo, kiongozi wa wachache bungeni, John Mbadi aliwaomba wabunge wengine kumpa nafasi Mohamud ya kusikilizwa na kujieleza.

"Tumpe muda. Huenda ana shida fulani na wazee. Kamati hiyo inatakiwa kumpa ushauri nasaha ili aweze kutambua kuwa hekima huja na umri," alisema Mbadi ambaye ni mbunge wa Suba Kusini.

Aliongeza kuwa marais wa zamani, Jomo Kenyatta na Mwai Kibaki waliingia madarakani wakiwa na umri wa zaidi ya miaka 70.

"Lakini licha ya kuwa na umri huo walitekeleza majukumu yao vizuri sawa na mwenzao Mzee Moi," alisema.

Mbunge wa Emurua, Dikirr Johanna Ng'eno ndiye pekee aliyeunga mkono pendekezo hilo la Mohamud.

"Huyu ni Mkenya jasiri ambaye anasema kile ambacho wengi wanaamini lakini wanaogopa kujitokeza hadharani," amesema  Ng'eno.

"Kuna baadhi ya watu ambao hutaka kubakia madarakani wakati ni wazi kuwa hawawezi kutekeleza wajibu wao ipasavyo kwa sababu ya kuwa na umri mkubwa. Mtindo huu sharti ukomeshwe."

Hata hivyo, Spika Muturi amewataka wabunge kutoa nafasi kwa kamati ya Cheptumo kushughulikia pendekezo hilo ipasavyo.

Naye Cheptumo amesema kwamba kamati yake itampa Mohamud muda wa kutosha ili aweze kuwasilisha hoja zake kwa njia huru.