Bunge laeleza jinsi wiza ya kilimo inavyoweza kuwa kipaumbele cha Taifa

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mahmoud Mgimwa

Muktasari:

Wadau wa kilimo wametakiwa kutoa maoni yao kwaajili ya marekebisho ya sheria na sera za kilimo ili kuweza kufanya wizara ya kilimo kuwa wizara ya kipambele

Musoma. Wadau wa kilimo nchini Tanzania wametakiwa kutoa maoni yao ili kuishinikiza Serikali kuifanya wizara ya kilimo kuwa miongoni mwa wizara zenye kipaumbele nchini.

Wito huo umetolewa leo Ijumaa Novemba 15,2019 na Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mahmoud Mgimwa kwenye mjadala ulioandaliwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la VI Agroforestry ikiwa ni sehemu ya maonyesho ya wadau wa kilimo mseto.

Amesema wadau hao wanapaswa kuishinikiza Serikali kupitia maoni yao ambayo hivi karibuni watatakiwa kutoa kufuatia serikali kuwa mbioni kufanya mabadiliko ya sheria na sera ya kilimo ambapo tayari sheria hiyo imesomwa bungeni mapema wiki hii.

Mgimwa amesema ili Serikali iweze kufanikiwa katika nia yake ya uchumi wa viwanda, wizara ya kilimo ni vema ikapewa kipaumbele kutokana na umuhimu wake huku akifafanua wizara hiyo ni miongoni mwa wizara ambazo zinaweza kutumika kwaajili ya uzalishaji wa mapato zaidi ya kutumika kama wizara ambayo inatumia mapato.

Amesema wizara hiyo pamoja na kuwa inategemewa na Watanzania zaidi ya silimia 70 lakini inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa maofisa ughani jambo ambalo linasababisha wakulima wengi kulima kwa mazoea hivyo kupata mavuno hafifu kila msimu.

" Tunataka malighafi kwaajili ya viwanda vyetu sasa hizo malighafi zitapatikana wapi kama sio kwenye kilimo na ili wizara hii iweze kuwa ya kipaumbele yapo mengi ambayo yanapaswa kufanyika ikiwa ni pamoja na kuwa na bajeti ya kutosha" amesema Mgimwa.

Amesema mbali na upungufu wa maofisa ughani lakini pia hata maafisa waliopo wamekuwa wakilazimika kufanya kazi ambazo sio za kwao na kutolea mfano kuwa sio ajabu kumkuta ofisa ughani wa kilimo akifanya kazi za afisa ughani wa mifugo jambo ambalo amedai kuwa linakwamisha maendeleo ya sekta hizo.

Pia, amesema umefika muda sasa maofisa hao wawe chini ya usimamizi wa wizara husika tofauti na ilivyo sasa ambapo maofisa hao wako chini ya Tamisemi huku akipendekeza kuwa endapo itashindikana maofisa hao kurudishwa chini ya wizara zao basi ziundwe Kurugenzi za kilimo, mifugo na uvuvi katika wizara ya Tamisemi.

Naye kaimu meneja wa VI Agroforestry, Thadeus Mbowe amesema umefika muda sasa Serikali inapaswa kuandaa sera ya kilimo mseto ili kilimo hicho kiweze kufanyika nchini na kuwa suluhisho la tatizo la mabadiliko ya tabia nchi.

Amesema kabla ya kuandaa kanuni kwaajili ya kilimo hicho cha mseto ni vema ikawepo sera ambayo ndiyo itakuwa mwongozo kwa wakulima hususan wadogo nchini.