Bunge lamthibitisha Dk Mpango kuwa Makamu wa Rais kwa kura 363

Bunge lamthibitisha Dk Mpango kuwa Makamu wa Rais kwa kura 363

Muktasari:

  • Wabunge 363 waliokuwepo bungeni mjini Dodoma leo Jumanne Machi 30, 2021 wamepiga kura za ndio kumthibitisha Dk Philip Mpango kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania.

Dar es Salaam. Wabunge 363 waliokuwepo bungeni mjini Dodoma leo Jumanne Machi 30, 2021 wamepiga kura za ndio kumthibitisha Dk Philip Mpango kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania.

Dk Mpango amethibitishwa baada ya kupendekezwa na Rais Samia Suluhu Hassan na jina lake kusomwa bungeni mjini Dodoma na Spika Job Ndugai.

“Naomba  kutangazia Bunge hili na nchi yetu kwa ujumla kwamba kura za hapana hakuna hata moja, kura zote 363 ni kura za ndiyo kwa hiyo amepata asilimia 100 ya kura zote.”

“Kufuatana na ibara ya 49 makamu wa rais  kabla ya kushika madaraka yake ataapishwa mbele ya Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kiapo cha uaminifu na pia kiapo kingine chochote kinachohusika na utendaji kazi wake kwa tarehe  itakayopangwa makamu wa rais mteule ataapishwa,” amesema Ndugai.

Katika ufafanuzi zaidi Ndugai amesema, “Katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania inatoa maelekezo kuhusu muda wa wabunge kushika madaraka yao, Ibara ya 71 inaorodhesha mambo ambayo mbunge atakoma kuwa mbunge au ataacha na miongoni mwa mambo hayo ni iwapo mbunge anateuliwa au kuapishwa kuwa makamu wa Rais.”