Bunge lataka kuwepo fungu ukarabati majengo ya Mahakama

Muonekano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kilichopo Buswelu mkoani Mwanza.

Muktasari:

  • Kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeitaka Serikali na Mahakama Kuu ya Tanzania kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kukarabati majengo ya Mahakama.

Mwanza. Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria wameitaka Mahakama Kuu ya Tanzania kutenga bajeti ya fedha kwa ajili ya ukarabati wa Mahakama jumuishi zilizojengwa nchini ili zitumike kwa muda mrefu.

Wakizungumza Machi 16, 2023 mara baada ya kutembelea na kukagua Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kilichopo Buswelu mkoani Mwanza, wajumbe hao wamesema angalau itenge fungu la ukarabati kila mwaka.

Mbunge wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi amesema kukarabatiwa kwa majengo hayo kutayafanya yadumu hivyo vizazi vijavyo kuendelea kupata huduma nzuri za kimahakama.

“Tumeisha pata jengo zuri hili, tusingependa kusikia mwakani tunaambiwa hatuna fungu la ukarabati, ni lazima rangi zitachubuka, ni lazima vifaa vilivyopo itafika wakati tutasema vitoke vije vingine,” amesema.

Ameeledelea kusema kuwa yapo majengo ya mkoloni yanayotumika mpaka leo ikiwemo Ikulu ya Dar es Salaam lakini hayajaachwa kwa sababu kuna fungu la ukarabati.

“Kwa hiyo ni eneo muhimu sana kuhakikisha tunatenga fedha za ukarabati kila mwaka ili majengo yetu yaendelee kudumu,”amesema Shangazi

Naye Mbunge wa Viti maalum CCM, Dk Alice Kaijage ameipongeza Serikali na Mahakama Kuu kwa kuweka chumba maalumu kwa ajili ya wanawake kunyonyeshea watoto wao huku akiomba majengo mengine ya mahakama yanayojengwa kufuata ramani kama ya kituo hicho.

Awali Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Leonard Magacha amesema kituo hicho kina ofisi ya Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mahakama ya Wilaya ya Ilemela ikiwemo ya watoto na Mahakama ya Mwanzo Buswelu.

Amesema kituo hicho kilichokamilika kwa gharama ya Sh8.5 bilioni kimesogeza huduma za Mahakama karibu na wananchi pamoja na kurahisisha uendeshaji wa shuguli za kimahakama kwakuwa wadau wote katika mnyororo wa utoaji haki wanapatikana katika jengo moja.

Naye Waziri wa Katiba na Sheria, Damas Ndumbaro amesema Serikali inaanza uboreshaji miundombinu ya Mahakama za Mwanzo na Wilaya Juni mwaka huu ili kuweka mazingira mazuri ya utoaji haki.

“Tunafahamu kwamba asilimia kubwa ya mahakama za mwanzo na wilaya haziko katika hali nzuri. Maeneo mengi ikiwemo Wilaya ya Ukerewe hazina hata miundombinu hivyo zinatumia majengo ya ofisi ya mkuu wa wilaya,” amesema

Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Florent Kyombo ameitakaa jamii na watumishi wa kituo hicho kukitunza na kuhakikisha kinakuwa katika mazingira mazuri.

“Ni wajibu wetu sisi ambao tunatumia haya majengo na vifaa vilivyomo kuvitunza ili vitusaidie kwa muda mrefu ujao,” amesema.