Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Burundi nayo yaitaja Hospitali Benjamin Mkapa muhimu kwa watu wake

Balozi wa Burundi nchini Tanzania Leontine Nzeyimana akizungumza na waandishi wa Habari na watumishi wa Hospitali ya rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa alipokwenda kuwatembelea wagonjwa toka nchini kwake

Muktasari:

  • Hiyo ni pili baada ya Serikali ya Malawi, kuitangaza hospitali hiyo kuwa miongoni mwa itakazopeleka wagonjwa wake.

Dodoma. Burundi imekuwa nchi ya pili katika ukanda wa Afrika Mashariki kuitangaza Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa (BMH) kuwa kituo muhimu cha matibabu kwa wananchi wake, hatua inayodhihirisha kuongezeka kwa imani ya mataifa jirani katika huduma za kibingwa zinazotolewa hospitalini hapo.

Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kuimarisha huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo na upandikizaji uroto, iliyofanikisha kukusanywa zaidi ya Sh2.2 bilioni.

Nchi ya kwanza kueleza hatua kama hiyo ilikuwa Malawi. Januari 16, 2026, Waziri wa Afya na Usafi wa Mazingira wa Malawi, Modalitso Baloyi, alitangaza kuwa Serikali ya nchi hiyo imeweka mkakati wa kuwapeleka baadhi ya wagonjwa wake kupata matibabu katika Hospitali ya Benjamin Mkapa.

Akizungumza leo, Ijumaa Julai 17, 2026, Balozi wa Burundi nchini Tanzania, Leontine Nzeyimana, amesema Serikali ya nchi yake imeridhishwa na kiwango cha huduma zinazotolewa hospitalini hapo, hususan ya moyo.

Amesema Burundi imewapeleka watoto sita katika hospitali hiyo kwa ajili ya matibabu ya moyo, watatu wamekwishafanyiwa matibabu na wanaendelea vizuri, huku wengine wakiwa katika hatua mbalimbali za kupatiwa huduma.

Nzeyimana, amesema uwezo wa wataalamu na vifaatiba vilivyopo hospitalini hapo umejenga imani kubwa kwa wananchi na Serikali ya Burundi.

“Tanzania na Burundi si ndugu wa wasiwasi, bali ni ndugu wa damu. Mwaka jana mlipokuja kutoa huduma Burundi, baada ya kuondoka wananchi wengi walionyesha masikitiko kwa sababu walikuwa wamefaidika na huduma muhimu za matibabu,” amesema.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Profesa Abel Makubi, amesema ujio wa wagonjwa kutoka Burundi umetokana na ziara ya kitabibu iliyofanywa mwaka jana na madaktari wa hospitali hiyo nchini humo.

Amesema katika ziara hiyo, madaktari wa BMH walifanya upasuaji kwa wagonjwa 50 na kutoa huduma mbalimbali za matibabu kwa zaidi ya wagonjwa 2,000 katika mikoa miwili walikoweka kambi za matibabu.

Profesa Makubi, amesema hospitali hiyo inaendelea kutekeleza mkakati wa kupanua huduma zake kwa nchi jirani kwa kutoa huduma zaidi ya 20 za kibingwa na ubingwa bobezi katika maeneo 17 ya tiba.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Gelasius Byakanwa amesema mafanikio ya hospitali hiyo yametokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika vifaa tiba na mafunzo ya wataalamu wa afya.

Hata hivyo, amesema bado kuna haja ya kuboresha huduma zinazowahusu wagonjwa na ndugu zao kutoka nje ya nchi, ikiwemo miundombinu ya malazi.

Ameeleza kuwa eneo kubwa la hospitali hiyo linaweza kutumika kujenga hoteli ya kisasa itakayosaidia kukuza utalii wa matibabu nchini.