Bwawa la Julius Nyerere lafikia asilimia 86

Muktasari:
- Mhandisi Mkazi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), Lutengano Mwandambo amesema shughuli ya ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 86.
Pwani. Mradi wa Kufua Umeme wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP), utakaozalisha megawati 2,115 umefikia asilimia 86, huku baadhi ya shughuli zikiwemo njia za maji ya kuendeshea mitambo na kituo cha kusafirishia nishati zikifikia ukingoni.
Hayo yameelezwa leo Jumanne Aprili, 25 2023 na Mhandisi Mkazi wa JNHPP, Lutengano Mwandambo wakati ziara ya Waziri wa Nishati, January Makamba alitembelea mradi huo kwa ajili kuangalia mwenendo ujenzi wake.
Mwandambo amesema hadi sasa shughuli ya kuchepusha maji imefikia asilimia 99.63 huku njia za maji ya kuendeshea mitambo ikifikia asilimia 99.08 na kazi ya kuchepusha mto asilimia 99.63.
Mbali na hilo, Mwandambo amesema kumekuwa na mwenendo mzuri wa maji kuingia katika bwawa hilo, akisema hata lile eneo la nchi kavu lililotumika na Rais Samia Suluhu Hassan katika uzinduzi wa kuyaruhusu maji, hivi sasa limefunikwa lote na maji.
"Disemba mwaka 2022 Wakati tunaanza kujaza maji katika bwawa hili mita za ujazo zilikuwa 71.5 kutoka usawa wa bahari, sasa hivi tumefikia mita 150.Hii ni hatua nzuri kwa sababu maji tunayahitaji kwa ajili ya kufua umeme katika mradi huu," amesema Mwandambo.
Kwa upande wake, Makamba amesema kumekuwa na mtiririko mzuri wa maji kuingia katika bwawa hilo, akisema hali ikiendelea hivyo kwa siku za usoni kutakuwa na maji ya kutosha ya kuzalisha umeme na watakuwa wakisubiria mashine kusukwa na kufungwa kwa ajili uzalishaji.
"Hali ambayo hupendi kuwa ni kwamba umeshamaliza kusuka na kufunga mashine za kuzalisha umeme umekunywa mikono unasubiri maji yajaye uanze kazi, lakini kwa mwenendo huu wa mtiririko mzuri wa maji hatukuwa na hali hiyo.
"Sasa hivi tupo mwezi wa tano tangu Rais Samia kubonyeza kitufue cha kuruhusu maji, bwawa hili linahitaji kuwa na lita bilioni 30, hadi sasa zipo bilioni sita ni kiwango kizuri.Hatukutarajia bwawa kujaa ndani ya msimu mmoja, lakini kumekuwa na matarajio makubwa," amesema Makamba.
Makamba amesema mandhari ya mradi yamebadilika, akisema hivi wanafikia hatua ya kutumia boti ndogo kwa ajili ya kukagua ujenzi mradi, jambo ambalo awali alikuwepo.
Amesema kazi zinakwenda vizuri na Serikali imeridhishwa na kasi ya uingiaji wa maji.
Hata hivyo, waziri huyo amesisitiza kuwa shughuli za kuanza uzalishaji wa umeme katika bwawa hilo, lenye thamani ya zaidi ya Sh6 trilioni itaanza rasmi Juni mwaka 2024.