Bwawa la Nyerere kuanza uzalishaji umeme

Muktasari:

  • Serikali imetangaza kuwa, wiki moja ijayo kina cha maji katika bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere (JNHPP) litakuwa na uwezo wa kuanza kuzalisha umeme.

Dodoma. Serikali imetangaza kuwa, wiki moja ijayo kina cha maji katika bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere (JNHPP) litakuwa na uwezo wa kuanza kuzalisha umeme.

 Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Mei 31, 2023 na Waziri wa Nishati, Januari Makamba wakati akiwasilisha bajeti yake kwa mwaka 2023/24 ambayo ameliomba Bunge lipitishe jumla ya Sh3.048 trilioni.

Waziri Makamba amesema kuwa ujazo wa maji uliofikiwa katika Bwawa hilo ni mita za ujazo 163, lakini kiwango kinachotakiwa bado mita za ujazo mbili.

Waziri wa Nishati, January Makamba akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2023/2024 leo Jumatano Mei, 31, 2023 jijini Dodoma.  Edwin Mjwahuzi

“Mheshimiwa Spika, ninafurahi kulitaarifu Bunge lako kuwa, wiki ijayo hata tukiamua kuanza uzalishaji wa umeme tunaweza kwani kiwango cha chini cha uzalishaji maji tumebakiza mita za ujazo mbili tu,” amesema Makamba.

Hata hivyo Waziri amesema kuwa uzalishaji wa umeme utakaoanza rasmi katika mwaka huu wa fedha, utaingizwa katika gridi ya Taifa mwakani sambamba na umeme wa jua.