Bweni lateketea ikifikisha matukio 30 ya moto Kagera

Baadhi ya wananchi wakiudhibiti moto uliokuwa unateketeza bweni la wanafunzi katika Shule ya Sekondari Omumwani Manispaa ya Bukoba. Picha na Alodia Dominick

Bukoba. Jumla ya matukio 30 ya majanga ya moto yameripotiwa mkoani Kagera kati ya Januari hadi Septemba, 2023 huku Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ikitaja makosa ya kiufundi kwenye mfumo wa umeme na hujuma kuwa miongoni mwa sababu za majanga hayo.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kagera, Zabron Muhumha, matukio sita moto kati ya 30 yaliyoripotiwa mkoani humo yanahusisha kuteketea kwa nyumba za watu binafsi na taasisi za umma zikiwemo shule.

Matukio mengine 24 ya moto yaliyoripotiwa mkoani Kagera ndani ya kipindi hicho yanahusu watu kuchoma misitu na mbuga.

Akizungumzia tukio la moto katika shule ya wasichana ya Omumwani uliotokea jana Jumapili, Oktoba 22, 2023, Kamanda Muhumha alisema japo jengo la bweni na mali zote zilizokuwemo zimeteketea, janga hilo halijasababisha madhara kwa maisha ya binadamu ukiachilia mbali wanafunzi 36 waliopata mshtuko na kukimbizwa hospitali kwa matibabu.

‘’Baadhi ya wanafunzi waliokimbizwa hospitali kutokana na kupata mshtuko tayari wameruhusiwa na wengine wanaendelea kupata huduma ikiwemo ushauri kuwaondolea hofu na kuwarejesha katika hali ya kawaida,’’ alisema Kamanda Muhumha

Alitaja baadhi ya mali zilizoteketea katika janga hilo ambalo chanzo chake kinaendelea kuchunguzwa ni nguo, madaftari ya wanafunzi na magodoro.

Alisema mabweni mawili yaliyoteketea katika tukio hilo hayafai tena kutumika kutokana na kuta zake kupasuka na kuhitaji matengeneza kabla ya kuruhusu kutumika tena na wanafunzi 124 waliokuwa wakiyatumia.


Mtukio mengine ya moto

Baadhi ya matukio ya moto yaliyotokea mkoani Kagera kwa mujibu wa Kamanda Muhumha ni lile la Mei 21, mwaka huu baada ya duka la magodoro la Ibrahim Karwani Soko Kuu mjini Bukoba kuteketea huku uchunguzi ukibaini sababu kuwa ni hitilafu kwenye mfumo wa umeme.

Tukio lingine ni la Julai 12, 2023 ambapo bweni la wavulana katika shule ya sekondari ya Istiqam liliteketea. Moto huo ulioteketeza mali zote za wanafunzi ulitokana hitilafu ya umeme.

Kamanda Muhumha alitaja tukio lingine kuwa ni Julai 4, 2023 ambapo watoto wawili, Mariam Mateso na Laurent Mateso waliteketea kwa moto uliounguza nyumba walimokuwa wakiishi huku tukio hilo likihusishwa na hujuma.

Kamanda Muhumha alitaja tukio lingine kuwa ni la Agosti 4, 2023 llililohusisa nyumba ya mtu binafsi lililoteketea na mali zote zilizokuwemo ndani.


Hatua zinazochukuliwa

Alisema kutokana na uchunguzi kubaini kuwa matumizi mabaya kwenye mfumo wa umeme na kutofanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye mfumo wa umeme kuwa miongoni mwa sababu moto katika matukio kadhaa.

“Tunatoa elimu kwa umma kupitia njia na majukwaa mbalimbali kuwezesha jamii kujikinga na majanga ya moto ikiwemo wamiliki wa nyumba kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ya mifumo ya umeme kwenye nyumba zao,’’ alisema Kamanda Muhumha

Alisema utoaji wa taarifa kwa wakati pindi janga la moto linapotokea ni eneo lingine muhimu linalotiliwa mkazo katika mafunzo na elimu kwa umma kuhusu kujikinga na majanga ya moto.