Bweni la wanafunzi lateketea kwa moto Bukoba

Baadhi ya wananchi wakiudhibiti moto uliokuwa unateketeza bweni la wanafunzi katika Shule ya Sekondari Omumwani Manispaa ya Bukoba. Picha na Alodia Dominick

Muktasari:

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Kagera, Zabron Muhumma amesema kuwa tukio hilo limetokea Saa 2:00 wa Oktoba 22, 2023.

Bukoba. Bweni la wanafunzi katika shule ya Sekondari ya wasichana Omumwani Manispaa ya Bakoba mkoani Kagera limeteketea kwa moto ambao chanzo chake hakijafahamika.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Kagera, Zabron Muhumma amesema kuwa tukio hilo limetokea Saa 2:00 wa Oktoba 22, 2023.

Amesema baada ya kupata taarifa, askari wa jeshi hilo kwa kushirikiana na wananchi walifanikiwa kuudhibiti moto huo kabla ya kusababisha madhara makubwa.

"Hakuna madhara kwa kibinadamu isipokuwa jengo na mali; chanzo cha moto huu hakijajulikana na tunaendelea na uchunguzi,’’ amesema Kamanda Mhumma

Alinda Benord, mmoja wa ashuhuda wa janga hilo amesema yeye pamoja na watu wengine waliojitokeza walijiahidi kuuzima moto huo kwa kutumia ndoo za maji na mchanga wakati wakisubiri ujio wa askari wa Zimamoto na Uokoaji.

Tukio la kuunguza bweni la wasichana shule ya sekondari Omumwani kuteteketea kwa moto limetokea miezi mitatu tangu tukio lingine la bweni la wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari Istiqam kuteketea kwa moto ambao chanzo chake hakikujulikana.