C-Pwaa ameondoka bila kutoa album yake

C-Pwaa ameondoka bila kutoa album yake

Muktasari:

  • Unalikumbuka kundi la muziki wa Bongo Fleva la Parklane ililotamba mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Dar es Salaam. Unalikumbuka kundi la muziki wa Bongo Fleva la Parklane ililotamba mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Wimbo Nafasi Nyingine ni kati ya nyimbo kali zilizoimbwa na wasanii wa kundi hilo, Suma Lee na Ilunga Khalifa maarufu C-Pwaa aliyefariki dunia usiku wa kuamkia jana Januari 17, 2021 katika hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa akipatiwa matibabu.

“Alikuwa kaka yangu na tulikuwa na uhusiano wa karibu sana mimi nikiwa mtangazaji na yeye msanii, tumeshirikiana kwenye vitu vingi sana,” anasema mtangazaji, Jabir Saleh ambaye alifanya mahojiano na C-Pwaa Juni, 2020.

“Kama kuna wasanii waliokuwa na hoja katika kuzungumza sambamba na umakini kwenye kazi basi C Pwaa ni miongoni mwao.”

Anasema Juni mwaka, 2020 alifanya naye mahojiano na baada ya hapo walikuwa wakiwasiliana kwa ukaribu huku msanii huyo akimueleza kuwa atatoa album yake mwanzoni mwa Januari, 2021.

 “Ukiachana na hayo C Pwaa alikuwa na mtazamo mzuri katika ukuaji wa sanaa yetu, alikuwa mzuri pia kwenye teknolojia ya habari na mawasiliano kwa hiyo unaweza kuona pengo aliloliacha,” anasema Jabir.

Anasema katika mahojiano yao waliichambua album hiyo na kimsingi ilikuwa na vionjo vya aina yake, “si unajua C Pwaa alikuwa mkali sana wa Crunk music. Yeye alikuwa wa kwanza kuleta mabadiliko ya aina ya muziki huo nchini na ndio maana alipewa jina la Kingo of Bongo Crunk.”

Kuhusu kundi la Parklane, mtangazaji  Jabir amesema, “lilikuwa kundi bora sana na nyimbo zao kuna muda zilikuwa kama na vionjo vya nyimbo za asili za mkoa wa Tanga na kwa kweli walileta utofauti mkubwa kwenye Bongo Fleva.”

Imeandikwa na Jabir Saleh mtangazaji wa radio ya EFM