CAG akubali yaishe, awaomba radhi wawakilishi
Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) Zanzibar, Dk Othman Abbas Ali
Unguja. Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) Zanzibar, Dk Othman Abbas Ali amekubali yaishe baada ya kuomba radhi Baraza la Wawakilishi kuhusu kauli aliyoitoa kwamba wajumbe wake hawana uwezo.
Katika mkutano wa jana, Spika wa baraza hilo, Zubeir Ali Maulid baada ya kipindi cha maswali na majibu alilieleza baraza hilo kwamba tayari CAG amekiri kuwa kauli yake ilileta taharuk, hivyo amekiri kwamba alikosea.
"CAG amekiri kuwa maneno yake yameleta tafsiri mbaya, hivyo amemuomba radhi mheshimiwa Spika wa Baraza la Wawakilishi, kamati ya PAC na kamati ya LAAC (Kamati za Kudhibiti Hesabu za Serikali) na wajumbe wote wa baraza hili kwa ujumla," alisema Spika Zubeir huku wawakilishi wakigonga meza kama ishara ya kupongeza.
Spika Zubeir alisema kutokana na kitendo alichokifanya CAG kufika katika ofisi za Spika na kutoa maelezo ya kuomba radhi kwa baraza, imemfanya (spika) akubaliane naye na ameridhishwa kutoa muongozo wake kama alivyoombwa.
Baada ya kutoa muongozo huo, Spika Maulid alisema kwa kuzingatia kanuni ya 64 (6) ya kanuni ya baraza la wawakilishi baada ya kutoa muongozo huo aliagiza kusitisha mjadala wowote ndani na nje ya Baraza la Wawakilishi.
"Mjadala huu umefungwa, itoshe tu kwa baraza hili kupokea taarifa ya CAG ya kuomba radhi na wajumbe mlichukue na kulipokea kama lilivyo," alisema.
Hatua hiyo ya kuomba radhi ilikuja baada ya wajumbe hao katika mkutano wa baraza hilo Juni 5, mwaka huu kuomba muongozo wa Spika wakimtaka CAG ombe radhi kwa kusema wajumbe wa baraza hilo hawana uwezo.
Muongozo huo uliombwa na Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Juma Ali Khatib aliyesema CAG alitoa kauli zinazoonyesha kulibeza na kulidharau baraza hilo hasa kupitia kamati zake kwamba hazina uwezo wa kufanyia kazi ripoti zake ikiwemo ripoti ya Tehama wakati CAG Abbas alipokuwa akiwasilisha ripoti ya ukaguzi ya mwaka 2021/22 Mei 3, mwaka huu Ikulu, Zanzibar.
Mwingine aliyechangia kuomba muongozo alikuwa Mwenyekiti wa Kamati la LAAC, Mwanaasha Khamis Juma na Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni ya Baraza la Wawakilishi, Mihayo Juma Nun’ga, ambao walisema katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ibara ya 5 imeeleza kuwa Taifa litakuwa na mihimili mitatu ikiwemo Serikali, Mahakama na Baraza la Wawakilishi bila kuingiliana.
Hata hivyo, siku moja baada ya wawakilishi kutaka muongozo huo wa kuliomba radhi, CAG alipotafutwa na gazeti hili ofisini kwake licha ya kudai hataki kuhojiwa na vyombo vya habari kuhusu masuala ya ripoti yake, alisema kwa ufupi kwamba wawakilishi hao wanajifurahisha.
Wakati akitoa kauli hiyo, kulibainika kwamba chanzo cha mzozo wake na baraza hilo kinatokana na uwasilishaji wa moja ya kitabu cha ukaguzi kukiandika kwa lugha ya Kiingereza ambapo ni kinyume na kanuni za baraza hilo.
Wakati akiwasilisha ripoti hiyo CAG alimuomba Rais Hussein Mwinyi kuzijengea uwezo kamati za Kudhibiti Hesabu za Serikali (PAC na LAAC) akisema hazina uwezo katika masuala ya Tehama, maana kuna vitabu vinne mpaka sasa kamati hizo zimeshindwa kuvifanyia kazi kwa kukosa utaalamu.
Katika kuliweka wazi zaidi, CAG alisema kamati hizo zimeshindwa kufanya uchunguzi wa mifumo ya Tehama ya Sh1.5 bilioni kwa Wizara ya Afya, Sh1.3 bilioni Wizara ya Ujenzi, Sh5 bilioni katika Wizara ya Fedha na zote zinahusu wizi katika mifumo ya Tehama.
Baada ya mwongozo huo wa Spika, gazeti hili lilizungumza na Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Khatib aliuesema wamepokea kama ambavyo Spika alisema na kutaka mjadala huo ufungwe.
"Kwa kuwa ameomba radhi baraza na kamati zake ni jambo la kiungwana kama Spika alivyosema tumeridhia na kitendo hicho," alisema Khatib ambaye pia ni mwakilishi wa kuteuliwa