CAG atonesha kidonda upigaji mabilioni

Muktasari:

  • Ni kwenye halmashauri, wadau washauri mbinu kukabiliana na upotevu fedha za umma

Dar es Salaam. Wakati viongozi wakuu wa nchi wakipigia kelele upotevu wa fedha katika halmashauri nchini, Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imethibitisha kutokusanywa Sh61.15 bilioni kutoka vyanzo muhimu.

Akizungumza jana Machi 28, 2024 wakati wa kukabidhi ripoti hiyo ya mwaka 2022/23 Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma, CAG Charles Kichere amesema zaidi ya Sh6.19 bilioni zilizokusanywa, hazikupelekwa benki.

Amesema pia mamlaka 184 za Serikali za mitaa hazikutenga Sh20.23 bilioni za mapato ya ndani kwa ajili ya miradi ya maendeleo na shughuli za uendeshaji.

Rais Samia akipokea ripoti ya CAG muda huu

Kutokana na hayo, wachambuzi wa siasa na wanasiasa wamehoji suala la uwajibikaji katika halmashauri, huku wakitaka Tehama itumike kufuatilia mapato na kubaini wizi.

Upotevu wa fedha umeripotiwa, wakati ambao Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakibainisha uchepushwaji wa fedha za halmashauri na udhaifu katika ukusanyaji wa mapato.

Kwa mujibu wa ripoti ya CAG ya mwaka 2021/22, kiasi cha mapato yasiyokusanywa kutoka kwenye vyanzo muhimu yalikuwa Sh37.34 bilioni.

Pia, ilionyesha mapato yaliyokusanywa lakini hayakufikishwa benki yamepungua ikilinganishwa na mwaka 2021/22, ambao ripoti ya CAG inaonyesha mapato hayo yalikuwa Sh11.07 bilioni.

Viongozi wa Wizara ya Nchi katika Ofisi ya Rais (Tamisemi), akiwamo Waziri Mohamed Mchengerwa, hawakupatikana leo Machi 29, 2024 kuzungumzia taarifa ya CAG, baada ya simu zao kuita bila kupokewa.

Hata hivyo, akizungumza katika mahojiano na Mwananchi hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Waziri Mchengerwa alisema tayari wizara imeanza kuwachukulia hatua wakiwamo watumishi wa ngazi za juu 35.

“Wapo ambao tumewashusha vyeo, wapo watumishi wengine maofisa wa kawaida tumewaondoa kwenye nafasi zao, wapo viongozi tumewaondoa nafasi zao na watumishi walioko mahakamani, ni wengi kesi zinaendelea,” alisema.

Kauli za Rais Samia, Majaliwa

Akizungumza baada ya kuwaapisha viongozi aliowateua Ikulu ya Dar es Salaam Machi 13, 2024, Rais Samia alisema fungu kubwa la fedha kutoka serikalini hupelekwa Tamisemi, ambalo mchango wake kurudi umekuwa mdogo, huku ukusanyaji wa mapato ukiwa mdogo.

“Nilikuwa naangalia taarifa ya mapato na matumizi na madeni kutoka Wizara ya Fedha, taarifa inasema kuwa, upande wa Serikali makusanyo ya kodi ni asilimia 97.7 upande wa makusanyo mengine hasa Tamisemi makusanyo yako asilimia 60 kwenda 70 kwa baadhi ya halmashauri,” alisema Samia.

Alisema halmashauri 15 zina makusanyo ya asilimia 50, akizitaka kwenda kujitazama na kuangalia sehemu wanayoweza kukusanya bila kuwabinya na kuwaonea wananchi.

Rais alisema kuna maeneo mengi ya fedha kwenye halmashauri ambazo zinaweza kukusanywa lakini zimeachwa zikipita na watu wengine wanazidaka.

“Kajiangalieni wapi mnaweza kukusanya bila kuleta usumbufu kwa wananchi,” alisema.

Aliwataka pia kusimamia mifumo ya ukusanyaji mapato kwa sababu ipo mitandao inayochepusha fedha za halmashauri.

“Lakini watu mpo huko mnaangalia, nashukuru Mbeya, ndiyo wamekuwa wa kwanza kutuambia jamani sisi tumeona hivi angalieni na kwingine kukoje, tunafuatilia huo mtandao, upo unaenda, wale wa huo mtandao wanaambiaza wanachepusha fedha nyingi sana,” alisema Rais Samia.

Ripoti ya CAG imetolewa ukiwa umepita mwezi mmoja tangu Waziri Mkuu Majaliwa alipomwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Salum Morcase kumkamata Mkuu wa Kitengo cha Fedha wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Saad Matunzi kwa tuhuma za kuhamisha Sh213.748 milioni kwa matumizi binafsi.

Majaliwa alitoa agizo hilo Februari 27, 2024 alipozungumza na madiwani na watumishi wa halmashauri hiyo mkoani Mara.

Akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Kigoma, Septemba 20 hadi 22, 2023, Waziri Mkuu Majaliwa alipata taarifa ya uwepo wa fedha zilizoingizwa kwenye akaunti ya Amana ya Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kutoka Tamisemi na kisha fedha hizo kuondolewa baada ya muda bila maelekezo maalumu wala kujua zilitumikaje.

Kwa mujibu wa timu ya uchunguzi, ilibainika Sh463.59 milioni zilitumwa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma na hazikuwa kwenye mpango wala bajeti ya manispaa na hazijawahi kuombewa matumizi kama bajeti ya ziada.


Maoni ya wadau

Kutokana na upotevu wa fedha za umma, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda ameshauri kuanzishwa kwa mfumo wa Tehama utakaowahusisha watendaji wa halmashauri, wizara, wakaguzi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

“Tuko kwenye karne ya sayansi na teknolojia, hivyo mfumo wa Tehama unapaswa kuongoza katika kuonyesha upitishaji wa fedha,” amesema.

 “Kuwe na ‘app’ (aplikesheni) itakayowahusisha mkurugenzi wa halmashauri, mkaguzi wa hesabu, wizara, Takukuru na hata CAG ili kuona tangu fedha zinapotoka wizarani, kuja chini na jinsi zilivyotumika. Mifumo iliyopo sasa haioni, ndiyo maana fedha zinapigwa,” amesema.

Amesema pia, baadhi ya watumishi wa Serikali si waaminifu; “ndiyo maana hii mifumo hutakuja kuiona ikiwekwa, kwa sababu wengi wanaamini wakishateuliwa ndio wametajirika.”


Hakuna uwajibikaji

Akizungumzia suala hilo, msemaji wa Serikali za Mitaa wa Bunge la Wananchi la Chadema, Mwaitenda Ahobokile ametaja sababu ya mapato kutopelekwa benki kuwa ni uhaba wa vifaa kama kompyuta na wataalamu wa kufundisha jinsi mfumo wa ukusanyaji wa fedha unavyofanya kazi.

“Upigaji upo kwa sababu kama watu hawana vifaa na hakuna wataalamu wa kutosha, basi wanachukulia ndiyo kisingizio na fedha hazipelekwi benki,” amesema Ahobokile.

Ametoa mfano wa taarifa ya Takukuru iliyoonyesha makusanyo ya Sh8.9 bilioni za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam zilizokusanywa kwa njia ya Pos, lakini hazikupelekwa benki, akihoji kutowajibika kwa waliohusika.

“Tulitarajia kusikia Rais Samia akiiagiza Takukuru iwakamate waliohusika washitakiwe, lakini hakuna uwajibikaji. Mtu anaona hata akifuja fedha za umma sana-sana atahamishwa au ataachwa tu,” amesema.

Msemaji wa Tamisemi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Kuluthumu Mchuchuli amesema bado kuna shida ya kufanya ukaguzi kama vile postmortem, akieleza mchakato huo unafanyika mambo yakiwa yameshaharibika.

“Yaani unafanya ukaguzi wa mwaka wa fedha uliopita, wakati upo mwaka wa fedha mwingine, ndiyo maana watu wanachukulia kitu cha kawaida kwamba, CAG ataandika kiasi cha fedha kilichopotea au kuliwa, halafu watasema ni hoja tu za ukaguzi na mwisho wahusika watazijibu kisha hoja zinakufa.

“Bado hatujalipa kipaumbele au kuamua ripoti za CAG zitusaidie kukabiliana na ubadhirifu, bado hatujaamua, badala yake tunafanya ili kuwa na ripoti za CAG kama vile utaratibu, kwamba usipofanya kuna vitu unaweza ukakosa kama nchi,” amesema Mchuchuli aliyewahi kuwa mbunge.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kuondoa Umasikini (Repoa), Dk Donald Mmari ametaja njia tatu za kukomesha upotevu wa fedha za halmashauri kuwa ni kuzijengea uwezo kwa kuongeza wataalamu wa ukusanyaji mapato.

“Waajiri wakaguzi wa ndani ambao hawatawajibika kwa mkurugenzi wa halmashauri, tofauti na sasa ili kudhibiti upotevu wa mapato. Pia, wanapaswa kuwachukulia hatua za kisheria wale wanaobainika kuhusika na ubadhirifu na watumishi wazembe,” amesema Dk Mmari.