CAG Kichere: Sitaki meno kuwang'ata wabadhirifu ninaowabaini

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG Charles Kichere wakati akisoma ripoti yake mbele ya waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dodoma Alhamisi, Aprili 6, 2023. Picha na Merciful Munuo

Dodoma. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amesema hana nia ya kuwa na ‘meno ya kung’ata’ kwa wanaokutwa na ubadhirifu kwenye kaguzi zao.

Kichere alisema katika utendaji mzuri ni muhimu kuwa na ‘check and balance’ (usawa) badala ya kukagua, kuhoji na kushitaki mwenyewe.

CAG alitoa kauli hiyo jana jijini Dodoma wakati akisoma muhtasari wa taarifa yake kwa waandishi wa habari muda mfupi baada ya ripoti zake kuwasilishwa bungeni.

Muhtasari huo unahusisha kaguzi 1,045 kutoka Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Mashirika ya Umma, vyama vya siasa na miradi ya maendeleo.

Hata hivyo, alionyesha mshangao kuwa taarifa ya ujenzi wa Chuo cha Ualimu cha Sumbawanga katika mradi wa EP4R kwamba ulitokea moto, lakini cha ajabu ziliungua nyaraka zenye thamani ya Sh632.5 milioni pekee.

“Nyaraka hizo zilikuwa sehemu ya matumizi ya Sh2.51 bilioni ambazo zilitolewa kwa ajili ya mradi huo na hadi sasa haijulikani kwa nini nyaraka pekee za fedha ndizo ziliungua na si kitu kingine,” alihoji Kichere.

Akijibu swali la mwandishi kuhusu anajisikiaje anapoona hakuna hatua zinazochukuliwa kwa watumishi waliobainika kuwa na mapungufu kwenye kaguzi zao, alisema kazi yake ni kukagua na kutoa mapendekezo kwa mamlaka husika ikiwemo Bunge ambao nao watakuwa na jukumu lingine kwa hatua zaidi, kazi aliyosema anaifanya kwa kufuata kanuni na miongozo.

Jana CAG alisisitiza kuhusu mzigo mkubwa walioubeba magereza wa kulisha wafungwa 3,110 wanaotumia Sh5.68 bilioni kwa mwaka kwa ajili ya kuwalisha wafungwa wahamiaji waliomaliza vifungo vyao.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali, Naghenjwa Kaboyoka alisema taarifa ya CAG itafanyiwa kazi na wahusika wataitwa mbele ya kamati Agosti mwaka huu.