Carlos alipua kituo cha redio Munich, Ujerumani (14)

Carlos alipua kituo cha redio Munich, Ujerumani (14)

Muktasari:

  • Katika toleo lililopita tulionyesha namna Carlos na Krocher-Tiedeman walivyomtuhumu Joachim Klein mbele ya bosi wao, Dk Wadi Haddad, kwamba alizembea wakati wa kuwateka mawaziri wa Opec mjini Vienna, Austria.

Katika toleo lililopita tulionyesha namna Carlos na Krocher-Tiedeman walivyomtuhumu Joachim Klein mbele ya bosi wao, Dk Wadi Haddad, kwamba alizembea wakati wa kuwateka mawaziri wa Opec mjini Vienna, Austria.

Mwishowe Dk Haddad alimfukuza Carlos kwenye chama cha PFLP kwa kushindwa kuwaua Yamani na Amouzegar.

Baada ya muda, Carlos aliondoka na Klein kwenda Yugoslavia Septemba 1976. Majasusi wa Ujerumani Magharibi waliigundua safari yake na kuwasiliana na wanausalama wa huko na alipofika huko akakamatwa na kuwekwa rumande.

Baada ya muda, Carlos na Klein walilazimishwa kupanda ndege kwenda Baghdad, Iraqi.

Akiwa huko, Carlos aliona nchi pekee ambayo angeweza kuishi kwa amani ni Yemen, kwa hiyo akaamua kuweka makazi yake Aden, ambako alianzisha kikundi kipya alichokiita ‘Organization of Armed Struggle’ kilichojumuisha waasi wa Syria, Lebanon na Ujerumani.

Alijenga pia uhusiano na polisi wa siri wa Ujerumani Mashariki waliojulikana kama ‘Stasi’ na walimpatia ofisi, watendaji 75, gari na walimruhusu hata kubeba bastola hadharani.

Kuanzia hapo Carlos alipoanza kupanga upya mashambulizi upya katika maeneo kadhaa ya Ulaya.

Mojawapo ya shambulizi ni lile la Februari 1981 alipolipua ofisi za Redio Free Europe (RFE) mjini Munich, Ujeruman

Shambulio hilo la Februari 21, 1981 lilitikisa jiji lote la Munich na kusababisha uharibifu mkubwa. Wafanyakazi kadhaa walijeruhiwa ingawa hakukuwa na vifo vilivyoripotiwa.

Tangu mwishoni mwa miaka ya 1970, Nicolae Ceausescu wa Romania aliendesha vita ya kulipiza kisasi dhidi ya RFE kwa sababu kituo hicho kilikuwa tishio kwa utawala wake.

Ceausescu aliwasiliana na Carlos na kumpa kazi ya kulipua kituo hicho cha redio.

Katika kundi la Carlos kulikuwa na magaidi wawili wa Kijerumani walioitwa Magdalena Kopp na Johannes Weinrich lakini walijulikana kwa majina ya Lilly na Steve.

Kwa kuwa kituo cha redio cha RFE kilikuwa kikimshambulia sana Ceausescu na Jenerali Pacepa alikitumia sana, mipango ilisukwa ya kukilipua.

Jumatatu ya Agosti 18, 1980, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Romania iliidhinisha kutekelezwa kwa mpango huo na kuuita NR. 225/f.9/0025323 dhidi ya mkuu wa idhaa ya Kiromania ya kituo hicho, Noel Bernard.

Ripoti ya siri iliyotolewa na idara ya usalama ya Mambo ya Ndani ya Hungary Oktoba 3, 1980 ilisema kulingana na mawasiliano ya simu waliyofuatilia kati ya Carlos na Sergiu Nica, iligundulika kuwa watu waliokuwa kwenye orodha ya Carlos ya kuuawa ni pamoja na Mhariri mkuu wa RFE, Emil Georgescu; Mfalme Michael aliyekuwa uhamishoni; mwandishi Paul Goma na wakimbizi wengine wa kisiasa.

Carlos alipewa pia kazi ya kuvunja na kuharibu kabisa kituo hicho na kuchukua nyaraka zozote za siri atakazozikuta humo.

Maofisa wa Romania walimpatia Carlos pasipoti 34 za kusafiria za nchi kama Ujerumani, Italia, Ufaransa na Austria pamoja na pasipoti za kidiplomasia kwa ajili yake mwenyewe, Weinrich na Magdalena Kopp.

Gaidi wa Uswisi aliyeitwa Bruno Breguet, akitumia jina bandia la Luca, aliungana nao Septemba 1980 kushiriki mkutano wa kulipua redio hiyo na ndiye aliyepangwa kutega bomu hilo.

Baada ya mjadala mrefu na kuahirisha mara kwa mara, walipanga kutekeleza nia yao usiku wa kuamkia Jumapili ya Februari 22.

Carlos akampigia Nica kumjulisha tarehe ya kulipua bomu. Alimwambia; “Steve atakuja Bucharest Jumapili asubuhi. Atakupigia simu saa 4 kamili asubuhi.”

Jumamosi usiku, Februari 21, 1981, magaidi wanne, Johannes Weinrich (Steve), Bruno Breguet (Luca), Jose Maria Larretxea (Schep) na mwanamke mwingine mmoja, walifika eneo la tukio wakiwa ndani ya gari lao aina ya ‘Ford’, wakaenda kutega bomu hilo katika kituo hicho, kisha wakatoweka.

Karibu na lilipotegwa, wafanyakazi watatu wa RFE walikuwa wakiandaa kipindi cha redio kilichokusudiwa kurushwa hewani saa nne usiku huo, lakini dakika kumi kabla ya kurushwa kwa kipindi hicho, bomu likalipuka na kusababisha uharibifu mkubwa. Ingawa hakukuwa na vifo kutokana na wafanyakazi wengi kutokuwapo usiku huo, majeruhi walikuwa kadhaa.

Kishindo cha mlipuko wa bomu kilisikika karibu eneo lote la jiji la Munich. Hata hivyo, mwaka mmoja baada ya shambulio hilo la bomu, Magdalena Kopp na Bruno Breguet walikamatwa mjini Paris wakijiandaa kwa shambulio jingine la kigaidi.

Gari lao lilipopekuliwa na polisi wa Paris lilikutwa na kilo tano za vilipuzi na ramani ya jiji la Paris.

Carlos aliitishia Serikali ya Ufaransa kuwa atalipiza kisasi iwapo watu wake wataendelea kushikiliwa na polisi.

Ili kuthibitisha hakuwa anatania, alifanya shambulio la bomu katika kituo cha treni iendayo kasi ya Paris-Toulon ambako watu watano waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Ufaransa, Jacques Chirac alikuwa amepangiwa kupanda treni hiyo lakini alighairi dakika chache kabla safari kuanza.

Siku ambayo kesi dhidi ya magaidi Kopp na Breguet ilikuwa inaanza, bomu lililotegwa kwenye gari lililipuka mjini Paris na kuua mtu mmoja na kuwajeruhi vibaya wengine 63.

Mahakama ya Ufaransa haikutishwa na matukio hayo. Iliendelea na kesi hiyo hadi hukumu ilipotolewa. Kopp alihukumiwa kifungo cha miaka minne na Breguet kifungo cha miaka mitano.

Carlos na kikundi chake waliendelea na shughuli zao za kigaidi dhidi ya maslahi ya Ufaransa.

Desemba 31, 1983 mabomu matatu yalilipuka mfululizo kwenye kituo cha reli cha Marseilles na kuua watu wawili na wengine zaidi ya 40 kujeruhiwa.

Mwezi huohuo bomu lingine lililipuka ndani ya treni ya mwendo kasi ya Ufaransa na kuua watu watatu na kujeruhi wengine wanne.

Januari Mosi, 1984 bomu lililipuka kwenye Kituo cha Utamaduni cha Ufaransa katika Jiji la Tripoli, Lebanon na kuua mtu mmoja.

Magdalena Kopp na Bruno Breguet waliachiwa huru kutoka gerezani nchini Ufaransa mwaka 1985.

Breguet alirudi Uswisi ambapo inaonekana aliachana na maisha ya kigaidi.

Kopp alikwenda kwanza Ujerumani na kisha Venezuela kukaa na familia ya Carlos. Je, nini mwanzo wa mwisho wa Carlos?


Tukutane toleo lijalo.