Catherine Ruge asimulia alivyoutosa ubunge 2020

Thursday June 10 2021
catherineeepiccc
By Peter Saramba

Catherine Ruge na Sharifa Suleiman ndio viongozi pekee wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) waliokosekana kwenye orodha ya wana Chadema 19 walioapa kuwa wabunge wa viti maalumu Novemba 24, mwaka jana, bila ridhaa ya chama hicho.

Walioapishwa siku hiyo ni Halima Mdee aliyekuwa mwenyekiti wa Bawacha na mbunge wa zamani jimbo la Kawe, Grace Tendega, Esther Matiko, Cecilia Pareso, Ester Bulaya, Jesca Kishoa, Nagenjwa Kaboyoka, Anatropia Theonest, Salome Makamba, Conchesta Rwamlaza.

Wengine walioapishwa na kuendelea kuwa bungeni licha ya Chadema kutangaza kuwavua uanachama tangu Novemba 27, mwaka jana ni Agnesta Lambart, Nusrati Hanje, Hawa Mwaifunga, Tunza Malapo, Asia Mohammed, Felister Njau, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala na Stella Fiao.

Pamoja na Mdee aliyekuwa Mwenyekiti, viongozi wengine wa Bawacha walioapa na nyadhifa walizokuwa nazo kwenye mabano ni Hawa Mwaifunga (Makamu Mwenyekiti Bara), Grace Tendega (Katibu mkuu), Asia Mohamed (Naibu katibu mkuu Zanzibar), Jesca Kishoa (Naibu katibu mkuu Bara) na Agnesta Lambart, uratibu na uenezi.

Katika kile kinachoonekana ni zawadi ya utii na uaminifu wao, Ruge na Sharifa wamekabidhiwa jukumu la kuongoza Bawacha kwa Ruge aliyekuwa mweka hazina kuwa Katibu mkuu huku Sharifa aliyekuwa Makamu mwenyekiti (Zanzibar) akitwaa mikoba ya Mdee ya kuwa Kaimu mwenyekiti.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu jijini Mwanza mara baada ya kuukwaa ukatibu mkuu wa Bawacha, Ruge alieleza alivyoruka viunzi vya ushawishi wa kujiunga na wenzake walioapishwa kuwa wabunge bila ridhaa ya chama.

Advertisement

Huku akizungumza kwa umakini na hisia, Ruge anasema taarifa za tukio la wabunge 19 wa viti maalumu kupitia Chadema zilisambaa kupitia mitandao ya kijamii, lakini alizipuuza baada ya kuwauliza waliokuwa wakitajwa, lakini wote walikana na yeye kuamua kuzipuuza akiamini ni uvumi wa mitandaoni.

Hata hivyo, anasema siku moja akiwa kwenye shughuli zake jijini Dodoma anakoishi, mmoja wa waliokuwa viongozi wa Bawacha (tunahifadhi jina kwa sababu hakupatikana) alimpigia simu kumjulisha mpango wa kupeleka majina NEC (Tume ya Taifa ya Uchaguzi) kwa uteuzi wa viti maalumu vya ubunge.

“Nilimuuliza iwapo suala hilo lina ridhaa ya chama; akaniambia hapana ila kuna mtu atawasilisha majina NEC hata kama Katibu mkuu hajasaini orodha hiyo. Kwanza sikuliamini hilo; pili nilimweleza kuwa siwezi kukisaliti chama na kwasababu tunayoipigania kwa miaka kadhaa,” anasimulia Ruge

Anasema baada ya simu hiyo aliwasiliana na viongozi wenzake wa Bawacha, wakiwemo aliokuwa akiwaamini na kuwachukulia kama mfano wa kuigwa na wote walikana kuwepo mpango huo na kwamba hayo ni maneno ya mitandaoni.

“Baada ya uhakika huo, niliwaamini wenzangu na kuendelea na shughuli zangu nikiamini maneno yale yalikuwa ya mitandaoni,” anasema.

Hata hivyo, ilipofika Novemba 17, 19, 20 na 21 taarifa hizo zilishika kasi na ilipofika usiku wa Novemba 23, mwaka jana orodha ya majina ya waliodaiwa kuwa tayari wako jijini Dodoma kuapa ilisambazwa mitandaoni, jina lake likiwemo.

“Kwa sababu orodha ile ilikuwa inasambazwa na mtu anayejiita Kigogo kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter, niliamua kumjibu pale pale kwenye ukurasa wake kuwa kamwe sitakisaliti chama changu na imani tuliyoipigania siku zote,” anasema Ruge huku akionyesha ujumbe huo wa Twitter

Katika ujumbe huo ulioandikwa saa 6:51 usiku wa Novemba 24, Ruge aliandika; “Am a loyal skeptical, That’s my character. A woman of principal, siwezi kusaliti chama changu. Nitakwenda bungeni kwa ridhaa na baraka za chama changu. Hizo nyingine ni story. Nimepitia maumivu makali sana mpaka sasa nina kesi na watu wa Serengeti wako bado ndani. Napata wapi ujasiri?”

Japo hajui kwa uhakika kwa nini jina lake liliondolewa iwapo ni kweli lilikuwepo kwenye orodha, Ruge anasema;

“Naamini msimamo wangu nilioonyesha kwa wote walionijulisha mpango huo, simu zangu na maswali kwa waliokuwa viongozi wenzangu wa Bawacha pamoja na ujumbe wangu kupitia Twitter zilitosha kuwapa ujumbe kuwa siko tayari kuisaliti imani yangu na chama changu.”

catherinepic

Ashindwa kulala siku mbili

“Asubuhi ya siku ya kuapishwa kwa wabunge 19 nilikuwa soko kuu mjini Dodoma kununua mahitaji ya nyumbani; mmoja wa maofisa wa Bunge alinipigia kuhoji kwa nini hanioni miongoni mwa wanajiandaa kuapishwa. Alinitajia waliokuwepo viwanja vya Bunge wakati huo. Sikuamini,” anasema Ruge.

Anasema kwa mshtuko alioupata, aliegesha gari pembeni kwa muda kuepuka ajali na alipotulia akaendesha hadi nyumbani na kukimbilia kuwasha luninga ili ashuhudie iwapo ni kweli. “Kweli nilipowasha TV nikakuta wenzangu ambao baadhi yao walikana kuwepo tukio hilo wakiapishwa,” anasema Ruge.

Anasema kutokana na imani aliyokuwa nayo juu ya waliokuwa viongozi wa Bawacha, hisia ya wahusika kukisaliti chama na imani waliyopigania kwa kipindi kirefu, tukio hilo lilimuumiza kiasi cha kukosa usingizi kwa siku mbili mfululizo.

“Baadhi ya walioapishwa wapo niliowaheshimu, kuwaamini na kuwachukulia kuwa mfano wa kuigwa kwangu, niliumia sana,” anafichua Ruge.

Kwa nini alikataa kuapishwa?

Ametaja sababu kadhaa za kuchukua msimamo wa kukataa kuungana na wenzake kwenda kuapa, ikiwemo kulinda imani yake ya haki, usawa na ustawi wa demokrasia nchini ambayo yeye na wenzake ndani ya Chadema wameipigania kwa muda mrefu.

Sababu nyingine ni kuheshimu na kuthamini hisia na imani ya wapigakura wa jimbo la Serengeti waliomuunga mkono wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu uliopita.

“Wana Serengeti wake kwa waume bila kujali tofauti zao kiitikadi waliniunga mkono katika harakati za kuwania ubunge; wapo ambao muda huo walikuwa ndani katika mahabusu ya polisi au magereza kwa kesi zilizotokana na uchaguzi; hivi ningetoa wapi ujasiri wa kusaliti imani hii kubwa? Siwezi na kamwe sitaweza,” anasisitiza Ruge.

Anaongeza; “Chama changu Chadema kimeniamini na kunipa fursa bila kujali uzoefu wangu mdogo kwenye ulingo wa uongozi wa kisiasa; natoa wapi ujasiri wa kwenda bungeni kuapa bila ridhaa ya chama?”

Uhusiano na walioapishwa

Akijibu swali kuhusu uhusiano wake na waliokuwa wabunge na viongozi wenzake, Ruge anasema; “Hatuna mawasiliano. Kuna kipindi nilikuwa naona status zao whatsapp lakini sasa wamenizuia. Binafsi siwachukii kama watu binafsi; bali nachukia usaliti wao kwa chama na kwetu tulioawaamini hadi kuwaona kama mifano ya kuiga.”

Bawacha mpya

“Bawacha tulipoteza viongozi wa juu sita baada ya waliokuwa viongozi kuwa kwenye orodha ya waliovuliwa uanachama kwa kuapa kuwa wabunge bila ridhaa ya chama. Uongozi mpya sasa tunalo jukumu la kuijenga upya baraza. Tuko tayari na tutafanya kazi hiyo kuanzia ngazi ya msingi hadi Taifa,” anasema Ruge akizungumzia nafasi yake mpya

Anataja jukumu lingine kwa uongozi mpya wa Bawacha kuwa ni kuihami katiba ya nchi kwa kuwashinikiza viongozi walioapa kuilinda na kutii viapo vyao ambapo wameanza na shinikizo kwa Spika Ndugai na NEC kuhusu wabunge 19 kuedelea kusalia bungeni licha ya kufukuzwa uanachama wa Chadema.

Kipaumbele kingine cha Bawacha kwa mujibu wa maazimio ya kikao cha kamati tendaji kilichokutana jijini Mwanza Mei 18 hadi 19 kuwa ni kudai Tume Huru ya Uchaguzi itakayowezesha chaguzi huru na haki.

Juhudi za Mwananchi kupata kauli kutoka kwa Mdee na wenzake jana zilishindikana baada ya simu yake ya kiganjani kuita bila kupokelewa na baadaye kutuma ujumbe mfupi wa maneno akiomba atumiwe ujumbe akisema alikuwa kwenye kikao; hata hivyo, ujumbe mfupi aliotumiwa haukujibiwa.

Hali ilikuwa vivyo hivyo kwa Ester Bulaya na Cecilia Pareso, ambao pia hawakupokea simu zao za kiganjani wala kujibu ujumbe mfupi wa maneno walizotumiwa.

Hata hivyo, alipozungumza kwa niaba ya wenzake muda mfupi baada ya kuapishwa Novemba 24, Mdee alisema walipata baraka za Chadema huku akimtaja mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Advertisement