CCM Hai yataka vitengo vya uchunguzi shuleni

Muktasari:

  • Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, kimeshauri kuanzishwa kwa vitengo vya uchunguzi shuleni na kuwapima watoto mara kwa mara ili kukabiliana na ukatili

Hai. Wakati matukio ya ukatili yaliyoripotiwa wilayani Hai, Mkoa wa Kilimajaro yakipungua kwa asilimia 52.94, kutoka matukio 68 mwaka 2022 hadi matukio 32 mwaka huu, Chama cha Mapinduzi (CCM) wilayani hapa, kimetaka uwepo wa vitengo vya uchunguzi shuleni.

Kwa mujibu wa CCM, vitengo hivyo vitatumika kama sehemu ya kuzuia vitendo vya ubakaji na ulawiti.

Ushauri huo umetolewa leo Jumanne, Desemba 12, 2023 na Katibu Mwenezi wa CCM wilayani hapa, Mohamed Msalu katika kilele cha siku 16 za kupinga ukatili ambapo amesema kuna haja ya watoto kupimwa mara kwa mara.

Amesema taarifa kutoka kwa maofisa elimu kuwa ukatili wanaofanyiwa watoto hugundulika wakati tatizo limeshakuwa kubwa.

Msalu amesema iwapo kutakuwa na kitengo cha uchunguzi shuleni, kutasaidia kupata taarifa mapema ambapo kama kuna tatizo linaweza kushughulikiwa na hivyo watoto kubaki salama.

Amesema: “Zamani wakati tunasoma, kulikuwa na tabia kuchunguzwa usafi wa nguo za ndani, jambo hilo lilikuwa zuri hata kama kuna tatizo unaweza kugundua na kulitatua mapema.”

Msalu ameendelea kusema: “Kwa hiyo vipimo vya mara kwa mara ni muhimu sana kwa watoto wetu ili kuendelea kuwalinda ili Taifa libaki salama kutokana hali ilivyo sasa."

Asifiwe James, ambaye ni Mkurungenzi wa Voice of Empowered Women Foundation, ametaka kamati za ulinzi na usalama kwa watoto ngazi ya Taifa, mikoa, wilaya, kata na kijiji; zifufuliwe na kwamba zinaweza kuwa suluhisho katika kupunguza au kumaliza tatizo hilo.

Naye Ibrahim Hamadi, aliyemwakilisha Sheikh wa Wilaya hiyo, Juma Lymo, amesema ukatili utapungua au kumalizika iwapo watu watakuwa na hofu ya Mungu na kuacha matendo maovu.

“Kumepigwa kelele sana, Serikali na wadau mbalimbali wamekuwa wakizungumzia juu ya hili, lakini vitendo hivi badala ya kupungua, vimekuwa vikiongezeka, ni vema sasa watu wakamgekia Mungu na kumcha,” amesema.

Awali katika taarifa yake Lucila Chima kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, amesema matukio ya ukatili mwaka 2022 yalikuwa 68 na mwaka huu yakiripotiwa matukio 32 sawa na kupugua kwa asilimia 52.94.