CCM kuanza Leo kutoa fomu za ubunge Ngorongoro

CCM kuanza Leo kutoa fomu za ubunge Ngorongoro

Muktasari:

  •  Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ngorongoro Mkoa Arusha, leo Oktoba 22 kimetangaza kuanza kutoa fomu za kugombea ubunge jimbo hilo ili kujaza nafasi ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, William Ole Nasha.


Arusha. Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ngorongoro Mkoa Arusha, leo Ijumaa Oktoba 22 kimetangaza kuanza kutoa fomu za kugombea ubunge jimbo hilo ili kujaza nafasi ya aliyekuwa mbunge William Ole Nasha.

Ole Nasha alifariki Septemba 27, 2021 jijini Dodoma baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Akizungumza kwa simu na Mwananchi leo, Katibu wa CCM wilaya ya Ngorongoro Amos Shimba amesema kuanzia leo Oktoba 21 hadi 24 itakuwa ni kuchukuwa fomu na kurejesha.

Shimba amesema Oktoba 25 itafanyika kura ya maoni ya wagombea ubunge na majina yataanza kujadiliwa Oktoba 26 na wajumbe wa sekretarieti ya wilaya, Kamati ya maadili na Kamati ya siasa.

"Baada ya kujadiliwa majina yatapelekwa ngazi ya mkoa na baadaye vikao vingine Kwa uteuzi wa mwisho," amesema.

Amesema taarifa za uchukuwaji fomu zitatolewa kwa wana CCM ambao wamejitokeza.

"Muda huu nipo ofisini nawasubiri wagombea ikifika saa 10 jioni nitakupa taarifa ambao wamejitokeza na tunawaomba wenye nia wajitokeza," amesema.

Amesema fomu za ubunge zitatolewa Kwa Sh100,000 Kwa wana CCM ambao wanajua kusoma na kuandika wenye umri kuanzia miaka 18.

Makada wa CCM wanaotajwa tajwa kuweza kumrithi Ole Nasha ni pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ngorongoro, Emanuel ole Shangai na aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Halmashauri, Elias Ngorisa na Mkurugenzi Mkuu Taasisi ya kudhibiti ubora wa mbegu (TOSCI), Patrick Ngwediagi.


Wengine ni Mratibu wa mashirika ya watetezi wa haki za Binadamu (THRDC), Wakili Onesmo Olengurumwa ambaye aliwahikuwa mjumbe wa baraza Kuu la umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wilaya ya Ngorongoro.

Wengine ni Mratibu wa miradi katika shirika la baraza la wafugaji  wanawake wa Ngorongoro(PWC), Alais Melau na mhadhiri Chuo cha Wanyamapori ya Mweka, Dk Kakoi Melubo, mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Saning'o ole Telele na mkurugenzi wa shirika la jamii ya wafugaji (TPCF), Joseph Parsambei.

Yumo pia Dk Elifuraha Laltaika, ambaye ni mhadhiri Mwandamizi wa sheria kutoka chuo Kikuu cha Tumaini Makumira ambaye aliwahi pia kuwa katibu wa hamasa wa UVCCM Ngorongoro na mjumbe Bodi mbalimbali za mashirika na shule.

Dk Melubo alipoulizwa kuhusu kutajwa tajwa huko na makada wenzake wa CCM, amesema hiyo imempa faraja na kuwashukuru wanaomhamasisha kugombea lakini akasema bado anatafakari na wakati muafaka ukifika ataliongelea hilo.

Kwa upande wake, Ole Ngurumwa alipoulizwa juu ya kutajwa kwake amesema ni jambo zuri wananchi kuthamini mchango wake katika jamii lakini wakati muafaka ukifika atazungumza

Kwa upande wake Parsambei amesema anashukuru Wananchi kutambua kazi anayofanya katika jamii huku Dk Laltaika akisema anashukuru kutajwa na ukifika wakati atazungumzia suala hilo Kwa kuzingatia maslahi mapana ya Ngorongoro.