CCM kukutana kupendekeza Rais Samia kuwa mwenyekiti wa chama

CCM kukutana kupendekeza Rais Samia kuwa mwenyekiti wa chama

Muktasari:

Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Humphrey Polepole amesema muda wowote kuanzia leo Jumamosi Machi 20, 2021 utafanyika mkutano mkuu maalum utakaokuwa na ajenda moja ya kupendekeza jina moja la Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mwenyekiti wa chama hicho tawala nchini Tanzania.

Dar es Salaam. Kamati Kuu ya CCM imekutana leo Jumamosi Machi 20, 2021 jijini Dar es Salaam kujadili ajenda mbili ikiwemo ya kujaza nafasi ya mwenyekiti baada ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania na mwenyekiti wa chama hicho, John Magufuli.

Mbali na nafasi ya mwenyekiti, nafasi ya katibu mkuu ipo wazi baada ya aliyekuwa akiishikilia, Dk Bashiru Ally kuteuliwa kuwa katibu mkuu kiongozi Februari 27, 2021.

Magufuli amefariki dunia Machi 17, 2021 katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu ya maradhi ya moyo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema mbali na ajenda ya kujaza nafasi hizo iliyoletwa na idara ya  oganaizesheni, pia wamejadili ushiriki wa chama hicho katika msiba wa Magufuli.

“Ajenda ya pili ilitoka idara ya oganaizesheni ilizungumza utaratibu, desturi na utamaduni wa CCM yanapotokea mazingira kama haya kwa sababu panahitajika zijazwe nafasi zilizo wazi,”

Amesema katika kikao hicho kilichoongozwa na makamu mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Dk Ally Mohamed Shein na makamu mwenyekiti Bara,  Philip Mangula kilihudhuriwa na viongozi wastaafu wa chama na Serikali wakiwemo marais wastaafu Ally Hassan Mwinyi na Jakaya Kikwete; Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na Waziri Mkuu mstaafu John Malecela.

Polepole amesema kamati kuu imeeleza kwamba ndani ya muda mfupi kuwe na mkutano mkuu maalum utakaopitisha jina la Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mwenyekiti wa CCM.

“Mkutano huu unatakiwa uandaliwe na ufanyike muda si mrefu kutoka leo. Kama ilivyo desturi yetu mkutano mkuu hutanguliwa na kikao cha halmashauri kuu ili kujaza nafasi,” amesema Polepole.

Kuhusu maombolezo ya kifo cha Magufuli, Polepole amesema  kamati kuu imeyajadili na kuwataka wananchi na wanachama wa chama hicho kujitokeza kwa wingi kuuaga mwili wa kiongozi huyo.

 “Leo hapa Dar es Salaam ilikuwa ni siku ya viongozi kuaga. Machi 21 ni kwa wakazi wote wa Dar es Salaam tunawaomba wanachama wetu tujitokeze kwa wingi,” amesema

Amesema Machi 22, 2021  wananchi wa Dodoma watapata fursa ya kuaga na Machi Machi 23 itakuwa zamu ya Wazanzibari, huku Machi 24 ikiwa ni kwa wakazi wa Jiji la Mwanza na mikoa ya Kanda ya Ziwa na Machi 25 itakuwa ni nafasi ya mkoa wa Geita na Wilaya ya Chato na maeneo ya jirani.

“Machi 26 kwa ratiba ya Serikali itakuwa ni siku ya kumpumzisha kiongozi wetu shupavu. Kamati kuu imeelekeza na chama kinatekeleza, wajumbe wote wa halmashauri kuu ya Taifa ya CCM ambao ni viongozi wenzake na Magufuli watashiriki shughuli ya mazishi kule Chato,” amesema Polepole.