CCM yajipambanua miaka 44 baada ya kuzaliwa kwake

Muktasari:
- Dk Bashiru asema madiwani, wabunge watakaokiuka maadili kuachwa njiani kuelekea 2025
Dodoma. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ali amewaonya wabunge na madiwani watakaokwenda kinyume na maadili na uadilifu, chama hakitasita kuwapoka uanachama wao.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi kuhusiana na miaka 44 tangu kuzaliwa kwa CCM, Dk Bashiru amesema wingi wa wabunge na madiwani una faida nyingi kuliko hasara, kwa sababu wanaweza kusimamia mipango yao bila kuyumba na kufika kila mahali.
Alisema anachotarajia kwa wingi huo, chama na serikali watafanya kazi kwa pamoja, lakini hata hivyo chama hakitapoteza jukumu lake la kuisimamia Serikali.
“Matarajio yetu hasa kupitia vikao vya kata na baadaye kwenda katika mabaraza yao ya halmashauri, wilaya na majiji na manispaa hawatasahau kuwa wako kule kuisimamia serikali,” amesema.
Amewakumbusha wabunge na madiwani wa CCM kuwa watapimwa kwa ukweli, uadilifu na uchapakazi.
“Awali tulikuwa tukiwapata madiwani ambao wako katika migogoro ikiwemo ya uvuvi haramu wakati chama katika ilani ya uchaguzi inasema itapigana nao,” ametahadharisha.
Anasema wapo baadhi yao walikuwa wakitumia nafasi zao kuhalalisha biashara zao wakati kanuni inawataka wasiwe na mgongano wa kimaslahi.
“Hili tutalisimamia kwa ukali sana linaweza hata kuwapotezea uanachama wao. Uzembe unaweza kumpa onyo na kadhalika lakini ukishachafua chama kutokana na kutokuwa mkweli, kuwa mzembe, haupatikani na haushirikiani na wananchi.
Hufanyi ziara halafu mbaya zaidi unavunja sheria unazotakiwa kuzisimamia, unashiriki kukwamisha ilani ambayo ndiyo umeitumia kujinadi, hilo linaweza kuwasababisha wapoteze uongozi baada ya kufutwa uanachama.”
Dk Bashiru anasema CCM kina kanuni za chama, kamati za madiwani na kamati za siasa za wilaya ambazo ndiyo wasimamizi wakuu wa kanuni na sheria za chama hicho.
“Haya makosa niliyoyasema yakidhihiri kabisa haijalishi wewe ni diwani wala mbunge utapoteza uanachama wako na ukipoteza uanachama utapoteza udiwani ama ubunge wako,” alisema.
Aidha, amesema ili kuleta mrejesho chanya, wabunge na madiwani watapimwa namna watakavyotekeleza ilani inayowataka kutenga muda kila wiki wa kusikiliza kero za wananchi na kuzifikisha kunakohusika na kuwarejeshea majibu.
Alisema wameandaa fomu ya tathimini kwa ajili ya kuwapima wabunge na madiwani na ipo idara mahususi inayoongozwa na Kanali Lubinga ambaye anasimamiwa na sekretarieti.
Alisema ni matarajio yao kuwa wao wenyewe kupitia kamati zao za madiwani na wabunge, watasimamiana kabla chama hakijaanza kuwasimamia.
Dk Bashiru alisema kwa upande wa wabunge kuna kamati ya wabunge wa CCM na mwenyekiti wao ni Waziri Mkuu ambaye pia ni mjumbe wa kamati kuu na kwamba, asipowasimamia atahojiwa kwenye Kamati Kuu ya CCM.
Kwa upande wa baraza la wawakilishi Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar ndiye mwenyekiti wa kamati ya wawakilishi Zanzibar.
Alisema vyombo hivi ni vya kikatiba na vyote vinasimamiwa na kamati kuu na kwa upande wa kamati za madiwani kamati hizo husimamiwa na kamati za siasa za wilaya na mkoa.
“Mfumo huo ndio utakaoamua nani tufike naye mwisho mwaka 2025 na nani atakwamia njiani. Lakini matarajio yangu ni kuwa kwa namna tunavyoenda kama timu moja hatutafika huko. Tutakuwa tunafanya ufuatiliaji wa mara kwa mara na kuwapa ishara kama mwelekeo unakokwenda sio mzuri ajirekebishe,” anasema.
Kamati iliyoundwa kuchunguza mali
Akizungumzia kamati iliyoundwa kuchunguza mali za CCM, anasema Desemba mwaka 2017 Kamati Kuu ya CCM iliunda kamati ya wajumbe tisa na yeye akiwa mwenyekiti wake na Mei 2018, ilianza kutoa taarifa zake za uchunguzi baada ya kukamilika.
“Taarifa hiyo ilibainisha changamoto za usimamizi wa maadili lakini pia matatizo ya kimaadili katika usimamizi wa mali za chama na hata kubaini baadhi ya mali hizo kuporwa na zingine kuwa hazina tija kwa usimamizi wake,” anasema Dk Bashiru.
Anasema mali hizo zilikuwa ni za chama pamoja na jumuiya zake na kwamba, kamati hiyo ilibaini kuwa chama kilishafanya marekebisho ya Katiba kwa kuunganisha mabaraza ya wadhamini wa jumuiya.
Anasema kabla ya mabadiliko hayo ya mwaka 2017, kila jumuiya ilikuwa na baraza lake la wadhamini yaani la Jumuiya ya Vijana, Wazazi na ya Wanawake. Hivyo, kulikuwa na mabaraza manne na kila baraza likisimamia mali kwa eneo lake.
Anasema utaratibu ule ulibadilishwa kikatiba na kuunda baraza moja na hiyo ikasaidia kuwa na baraza moja imara la wadhamini linalosimamia mali za chama pamoja na jumuiya zake.
“Kwa hiyo Kamati ilipobaini hayo, ilitoa mapendekezo ambayo yalipitishwa na Kamati Kuu. Sasa inaelekea miaka mitatu tangu kamati hiyo itoe taarifa yake na katika maagizo ya Halmashauri Kuu, ilikuwa kila jumuiya na vyombo vyake vya uongozi vikatekeleze mapendekezo yanayohusu maeneo yao,” anasema Dk Bashiru.
“Napenda kutaarifu kwamba mapendekezo mengi yamefanyika, tumefanya kazi nyingi ambazo ni za chama na tumebaini kwamba thamani ya mali za chama ilikuwa haijulikani wakati huo.”
“Tulibaini mali zilikuwa na thamani isiyozidi Sh60 bilioni lakini baada ya tathimini chama kinaelekea kuwa na mali zenye thamani ya zaidi ya Sh1 trilioni.”
Katibu Mkuu huyo anasema wameweka mfumo wa usimamizi wa fedha na kanuni ya fedha, sasa kila senti inayoingia kwenye chama inawekwa katika mfumo wa kidijitali na wanaoweka benki wanatumia namba maalumu ya malipo.
Hali hiyo imewawezesha kujitegemea bila kuomba msaada wa mtu katika uchaguzi mkuu wa 2020 tofauti nai chaguzi zingine zilizopita.
Anasema mali zote za CCM zilizopotea tayari wamezirejesha ikiwamo ardhi, majengo, magari na mitambo ambavyo sasa vinakiingiza chama mapato ya kutosha.
Nini kinafanyika hivi sasa
Katibu mkuu huyo anasema kwa sasa chama chao kinaendelea kupanua wigo wa wawekezaji wenye tija na kuondoa usio na manufaa kwa chama.
“Tunafanya pia mafunzo ya wasimamizi ili wawe na uelewa kwa sababu tumeweka mifumo ya kisasa ya usimamizi wa mali zetu,” anasema Dk Bashiru.
Lakini pia anasema ili kufanikisha yote haya, CCM kinaendelea kuwahimiza wanachama kuendelea kuwa na moyo wa kujitolea kwa sababu uchumi wa chama hauimarishwi tu na miradi ya kiuchumi, bali pia na michango ya wanachama ya hiari.
Kadi za kieletroniki
“Tunafanya uhakiki wa kina kwa kusajili wanachama kielektroniki ili tuwe na taarifa za uhakika kwa sababu chama chetu ni kikubwa sana. Tuna matawi zaidi ya 24,000 na kule ndiko wanachama wanakopata uanachama.
“Kule chini mfumo wake wa kutunza taarifa si mzuri sana kwa sababu kazi za kule ni za kujitolea. Kwa hiyo utunzaji wa taarifa unakuwa ni wa makaratasi tu, hivyo kuzichambua kisha uhakiki inachukua muda.”
Anasema mfumo huo wa usajili utazinduliwa rasmi mwezi huu Jijini Dodoma ambako watagawa kadi za kielektroniki kwa wanachama wao.
Anasema kadi hizo zitasaidia sio tu kujua taarifa binafsi za mwanachama, bali pia ulipaji wa ada na kujua idadi sahihi ya wanachama wao nchi nzima.
Anasema kufanya hivyo si kwamba CCM kimejiamulia tu, lakini pia ni takwa la Sheria ya Vyama vya Siasa inayowataka wawe na madaftari ya wanachama.
“Kwa hiyo sio tu tunatekeleza jambo hili kama njia yakuboresha mifumo yetu ya ndani ya chama, lakini ni takwa la sheria ambalo litawasilishwa kwa msajili,” anasema.
Alisema wametoa vitambulisho mabalozi wote na watumishi wote nchi nzima na kutoa wito kama kuna maeneo ambayo mabalozi hawajapata vitambulisho vya uongozi wajitokeze.
Alisema wanajumla ya malozi 250,000 nchini nzima na hivyo kuwafanya kuingia katika mfumo wa kidijitali zinazoonyesha taarifa zao.
Hata hivyo, alisema mpaka sasa wanachama zaidi ya millioni 10 kwa takwimu tulizonazo na kwamba wanaweza kuwa zaidi.
Alisema mfumo wa kidijitali utawaonyesha hata jinsi ya uanachama wao, viwango vyao vya elimu, maeneo yao wanakotoka, kazi zao na umri wao na hivyo kuwapa picha kamili kuhusu sifa hasa za uanachama wa chao.
Alisema pia katika eneo la kiuchumi wanataka kufanya tathimini ya mali hizo ambazo wamezirejesha kwa sababu hesabu iliyopo hivi sasa ya Sh 1trilioni ni ya mali zote zilizorejeshwa na zile ambazo zilikuwepo kwa wakati huo.