CCM yataka mfuko walioathiriwa na wanyamapori

Muktasari:
- Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo ameelekeza kuundwa kwa mfuko wa fidia kufuatia malalamiko ya wananchi kuvamiwa na tembo wanaoharibu mazao yao mashambani.
Kiteto. Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo ameelekeza kuundwa kwa mfuko wa fidia kwa uharibifu unaofanywa na wanyamapori katika vijiji vyao ili waathirika wa uharibifu huo walipwe stahiki zao mapema.
Chongolo ameeleza hayo leo Machi 9, 2023 katika kijiji cha Ndaleta kilichopo wilayani Kiteto baada ya kupokea malalamiko ya wananchi kuhusu uharibifu unaofanywa na tembo kutoka hifadhi ya Taifa ya Tarangire wanaovamia mashamba yao.
Akiwa katika kijiji hicho, wananchi wamelalamikia kuvamiwa na tembo ambao wanaharibu mazao yao mashambani, jambo ambalo linawafanya wakose chakula na kutolipwa fidia zao kwa uharibifu huo.
"Tembo wamekuwa ni changamoto kubwa kwetu, wanaharibu mazao yetu na tukilalamikia kulipwa fidia hatulipwi. Mwaka 2021 tathmini ilifanyika lakini hatujalipwa hadi leo," amesema Athumani Ramadhani, mkazi wa Kijiji cha Ndaleta.
Kwa upande wake, Abdallah Mfaume amelaamikia kunyanyaswa na maofisa wa hifadhi hiyo ambao wamekuwa wakiwazuia kwenda kwenye mashamba yao na kutowalipa fidia ya uharibifu unaofanyika.
"Tunaomba utusaidie, tembo wamekuwa ni kero kubwa katika kijiji hiki, tuna hofu pia ya usalama wetu tunapokwenda mashambani. Tunataka tulipwe fidia, tuna watoto tunasomesha na kuwalisha, sasa kama mazao niliyolima yameharibiwa nitaishije na familia yangu?" amehoji.
Akijibu changamoto hiyo, Chongolo ameeleza haja ya kuundwa kwa mfuko maalumu wa fidia kwa uharibifu unaoletwa na wanyamapori ili fedha za fidia ziwepo wakati wote na zilipwe kwa waathirika kwa wakati.
Ameeleza kwamba mapato ya hifadhi ya kiwango fulani kama asilimia 0.03 yanakuwa yanawekwa kwenye mfuko huo na kunakuwa na kamati maalumu ya kuhakikisha kwamba wananchi wanalipwa fidia inayostahili na inayoendana na hasara aliyoipata.
"Kamati hiyo ihusishe wataalamu wa hifadhi na wajumbe kutoka vijiji vinavyozunguka hifadhi. Wajumbe hao watokane na mkutano mkuu wa kijiji, kwa hiyo tafuteni watu sahihi wa kuwawakilisha ili wakawasemee vizuri," amesema Chongolo.
Amesisitiza kwamba anakwenda kuhimiza jambo hilo kwa Waziri wa Maliasili na Utalii ili litekelezwe na kumaliza adha hiyo inayowakabili wananchi na kuwasababishia upungufu wa chakula.