CCM yatoa maagizo utanzaji vyanzo vya maji

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo akizungumza na wananchi wa eneo la kijiji cha Kisiwani Wilayani Muheza leo wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani humo.

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo ameendelea na ziara yake Mkoa wa Tanga yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Ilani ya chama hicho kwa mwaka 2020/25.

Muheza. Wataalamu wa mazingira nchini Tanzania wametakiwa kutengeza mpango maalumu wa kuvitambua vyanzo vipya vya maji kote nchini humo na kuviwekea mkakati wa kuvilinda na kuvitunza kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo leo Alhamisi, Agosti 11, 2022 wilayani Muheza Mkoa wa Tanga, alipokuwa akizungumza na wananchi wanaoishi vijiji vilivyopo jirani na hifadhi ya msitu wa Longuza.

Amesema kwa sasa kumekuwa na changamoto kubwa ya mabadiliko ya tabianchi yanayotokana na shughuli za kibinadamu zinazosababisha uharibufu wa mazingira hivyo wataalamu wawe na mikakati yakinifu ya kuvitambua vyanzo vipa na kuweka mikakati ya kuvilinda na kuvitunza.

"Wataalamu msibweteke tu maofisini, tukafanye kazi hasa ya kuibua vyanzo vipya vya maji hali ni mbaya kutokana na uharibifu wa mazingira, tukuchukue hatua sasa," amesema Chongolo.

Pia, Chongolo amewasisitiza wananchi katika suala zima la utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji vilivyopo ili kujiepusha na janga la ukame litakalosababisha upungufu wa maji.

"Mfano kufanya shughuli za kilimo katika vyanzo vya maji na machimbo ya madini katika maeneo haya pamoja na ukataji wa miti hivyo haya yote yatatupeleka kwenye ukame," amesema Chongolo.

Chongolo yupo mkoani Tanga katika ziara ya kikazi ikiwemo kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kukutana na wanachama wa chama hicho katika Wilaya za Muheza, Pangani ,Tanga, Lushoto na Mkinga.