CCM yawakalia kooni viongozi wazembe Pwani

Muktasari:

  • CCM yasema wapo baadhi ya viongozi mkoani Pwani wanashindwa kuakisi matakwa ya katiba na kikanuni ya chama hicho, hawawajibiki kwa watu wanaowaongoza

Kibaha. Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC), Organaizesheni Taifa, Issa Haji Ussi Gavu amesema CCM imepata taarifa ya kuwapo baadhi ya viongozi wa vijiji, vitongoji na mitaa mkoani Pwani wanaoshindwa kuwajibiki kwa watu wanaowaongoza na kusema viongozi hao hawahitajiki ndani ya chama hicho.

Pia amesema wapo baadhi ya wabunge na madiwani wameanza kuhangaika na kupanga safu za watendaji wa vijiji, vitongoji na mitaa kwa lengo la kusaidiwa kwenye kura za maoni mwaka 2025 na kuwataka wote wasipoteze muda kwa sababu chama hakipo tayari kwenda na viongozi wasiowapigania wananchi.

Gavu amesema hayo jana Jumapili, Novemba 26, 2023 alipozungumza  kwenye baraza la wazee CCM mkoani Pwani katika kikao kilichohudhuriwa na wawakilishi wa wazee kutoka  halmashauri zote mkoani humo.

Amesema katika uchaguzi ujao hakuna sababu ya kupanda mlima wakati vichuguu vipo, watatafutwa watu wanaouzika, wanaokubalika na watakaosaidia chama hicho.

"Tunahitaji kumuona mwenyekiti wa kijiji, kitongoji, mtaa, diwani na mbunge aliye tayari kuhangaika na mambo ya watu anaowaongoza, kwa hiyo tafutieni watu nafasi ya uongozi watakaokwenda kusimama kuhangaika na mambo ya watu wanaowaongoza na sio mambo binafsi," amesema.

 Amesema katika misingi ya kuimarisha chama hicho kiujumla, baraza la wazee lina mambo ya msingi ya kufanya, ili chama kiende vizuri na kutaja mojawapo ni kuwakumbusha viongozi waliopo madarakani kurudi kwenye utaratibu wa kikatiba na kikanuni wa chama hicho na kuitisha vikao.

Amesema kumekuwa na tatizo kubwa la viongozi wa chama hicho kukaa na kutotimiza matakwa ya kikanuni ikiwemo uitishwajii vikao na hivyo chama kushindwa kupata uhalisia wa matatizo ya wananchi.

" Niwasihi wazee wangu ninyi kwa mujibu wa katiba ya CCM ibara ya 124,  ninyi ni taasisi na kikao halali ndani ya vikao vya chama hivyo rudini mkasimamie kanuni ya wazee taleo la 2019 ibara ya tatu inaelekezea madhumuni na umuhimu wa baraza la wazee kwa ngazi husika," amesema na kuongeza.

"Kwa hiyo niwasihi na niwaombe msione tabu wala shida kurudi kwenye ngazi husika mkatoe ushauri kwenye vikao husika tukawakumbushe viongozi wetu warudi kwenye utaratibu wa kuitisha vikao

ili mambo yaende vizuri, mkichekea kusema au kushauri huko mtakuwa hamkitendei haki chama, Taifa letu na nafasi na fursa mliyopewa na katiba yetu," amesema.

Amewaeleza wazee hao kuwa wasipotekeleza fursa yao ya kikatiba mambo yakienda vibaya kwenye chama hakuna namna na wao kukataa lawama hizo na watabeba msalaba huo wa kutokushauri, kutowaelekeza, kutowaongoza na kutotoa malekezo kwa viongozi ngazi mbalimbali ili mambo yanyooke.

Aidha amewaeleza wazee hao kuwa wamepewa nafasi ya sehemu ya kwenda kusimamia utekelezaji na miongozo sahihi katika kupata viongozi wazuri wa Taifa hili hivyo kwa kushirikiana na halmashauri kuu za Wilaya wakasimamie haki kwa kuishauri kuhakikisha haki inatendeka na pia waliomadarakani wanatimiza wajibu wao.

"Ili tushinde uchaguzi uliombele yetu tunahitaji tuwe na umoja, mshikamano na uzalendo na kwamba umoja na mshikamano huo utatokana na umoja na kuelewana kwetu kwenye vikao tunapojadili mambo yetu kwa hiyo wazee wangu tusione tabu wala shida ndio sehemu pekee na sahihi ya kusema mawazo yako, mchango,hisia zako ili wenzako wasikie wajadili wapime na mwisho wa siku mtakubaliana na kutoka mkiwa wamoja," amesema.

Ameongeza kuwa kwa bahati mbaya wapo baadhi ya viongozi wenzao kwenye vikao wanataka kugeuka miungu wanataka wanalolitaka wao ndiyo liwe hilo hilo wakati kwenye  CCM jambo hili alina nafasi na kwamba chama hicho ni cha demokrasia na kwenye hilo lazima itengenezwe daraja na foramu ya watu kuzungumza.

"Nikuombe Mwenyekiti wa CCM mkoa mjue kuwa kwenye chama hiki hatuna deni la Mbunge, diwani au mwenyekiti wa Kijiji, kitongoji na mtaa hawa wote tuna wajibu wa kuwalinda kuwatetea kutimiza matakwa yao lakini utetezi huo usitumike kama fimbo ya kuwaadhibu wengine," na kuongeza.

“Wabunge hao nao ni binadamu inawezekana utashi wao ukapelekea kuumiza wengine hakikisheni mnailinda demokrasia, mnalinda haki na mnasimamia wajibu wa kikatiba na kikanuni." 

Awali, wazee hao walianza kikao kwa kutoa maoni na ushauri wa mambo mbalimbali ambapo mengi wameomba kuboreshwa kwa madirisha ya dawa kwenye vituo vya afya na hospitali kwani mengi yamekuwa yapo kwa jina tia lakini huduma ya dawa mbalimbali hakuna zaidi ya Panadol.

Ingine ni wameomba Serikali kukamilisha miundombinu ya barabara kwa kiwango cha la lami njia zinazoungaisha wilaya za Mkoa wa Pwani kwani kwa sasa hakuna njia ya usafiri wa uhakika ya ndani ya mkoa kutoka wilaya moja kwenda ingine na kuboreshwa huduma ya upatikanaji nishati ya umeme.

Hata hivyo, kikao hicho pia kilitoa pongezi kwa namna Serikali awamu ya sita inavyoelekeza nguvu katika kutatua kero za wananchi hasa katika sekta ya elimu, afya na maji.

Kamisaa wa CCM Pwani, Abubakari Kunenge ameelekeza kuwa katika kipindi cha miaka miwili 2021/ Juni 2023 ya Serikali awamu ya sita kuingia madarakani takriban Sh1.2 trilioni zimepokelewa mkoani humo kwa ajili ya utekelezaji shughuli na miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya maji, umeme, elimu, afya, miundombinu ya barabara.