Chadema: Bodaboda achaneni na Lowassa

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa akihutubia mkutano wa Operesheni Pamoja Daima katika mji wa Namtumbo mkoani Ruvuma juzi. Picha na Mpiga Picha wetu

Muktasari:

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amevishukia vyombo vya dola kwa kuvitaka kufanya kazi kwa weledi.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeendelea na Operesheni Pamoja Daima katika mikoa mbalimbali nchini.

Kyela. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewataka madereva wa pikipiki zinazobeba abiria maarufu kama `Bodaboda’ kuacha kumuunga mkono Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa.

Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika jana kwenye Uwanja wa Siasa ulioko mjini Kyela, Mbunge wa Mbeya Mjini kupitia chama hicho, Joseph Mbilinyi aliwashauri watu wa bodaboda kupokea misaada ya kiongozi lakini ikifika uchaguzi waichague Chadema.

Sugu, ambaye alikuwa amefuatana na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa ikiwa sehemu ya Operesheni Pamoja Daima ya chama hicho, alisema kuwa Lowassa anatafuta kuungwa mkono na makundi mbalimbali ili kufanikisha malengo yake ya urais.

“Lowassa katika siku za karibuni amekuwa akitoa misaada mingi kanisani sasa amehamia kwenye bodaboda,” alisema Sugu huku akishangiliwa na umati mkubwa wa watu uliofurika kwenye mkutano huo.

Sugu alisema kuwa bodaboda wanapaswa kuachana na Lowassa kwani ni mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho hakina msaada kwao.

“Akiachana na CCM, akaamua kwenda chama kingine basi mnaweza kumuunga mkono ila akibaki CCM achaneni naye,” alisema Sugu wakati akimzungumzia Lowassa, ambaye hivi karibuni alishiriki katika bonanza lililoandaliwa na Bodaboda jijini Dar es Salaam.

Mapema Dk Slaa na Mchungaji Msigwa waliendesha operesheni hiyo kwa kupaa kwa helikopta jana asubuhi hadi wilaya za Ludewa, Makete, Rungwe na Kyela huku wakiwekea mkazo masuala ya matatizo ya ufisadi, matumizi mabaya ya rasilimali na vita dhidi ya ujangili.

Lissu avishukia vyombo vya dola

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amevishukia vyombo vya dola kwa kuvitaka kufanya kazi kwa weledi.

Akihutubia kwenye Uwanja wa Kiboroloni mjini Moshi, Lissu alisema kuwa matukio ya polisi kuua raia na hata madhara yaliyotokea kwenye Operesheni Tokomeza Ujangili yanatokana na matatizo yanayokabili vyombo vya dola.

“Angalia matatizo yanayokabili Jeshi la Polisi kama makazi na masilahi duni ndiyo yanachangia wao kuua raia,” aliongeza Lissu.

Mnyika, Lema waunguruma

Pia viongozi wa Chadema waliendesha kampeni yao katika mikoa ya Tabora na Katavi kwa kuhutubia Sikongwe, Mpanda Mashariki, Mpanda Magharibi na Mpanda mjini.

Viongozi walioshambulia jukwaa ni pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Chadema kwa upande wa Zanzibar, Said Issa Mohamed, Mkurugenzi wa Uenezi wa chama hicho, John Mnyika, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.

Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, aliwashutumu viongozi wa Serikali kuwa wamekuwa wakitumia vibaya rasilimali za nchi na kusababisha Watanzania kuendelea kuwa masikini, huku wachache wakinufaika.

Naye Lema alizungumzia juu ya timuatimua iliyowakumba viongozi kadhaa wa chama hicho akiwataka wananchi waamini kuwa Chadema ni makini na kamwe hakitawavumilia wasaliti.

Imeandikwa na Raymond Kaminyonge (Kyela), Rehema Matowo (Moshi) na Mussa Mwangoka (Mpanda)