Chadema kuishi bila ruzuku, yaibuka na mkakati mpya

Chadema kuishi bila ruzuku, yaibuka na mkakati mpya

Muktasari:

  • Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza kuanza utekelezaji wa mpango wa kujiendesha kwa mapato yake kikitumia taarifa za kidigitali za wanachama wake maarufu kama ‘Chadema Digital.’

Dar/Arusha. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza kuanza utekelezaji wa mpango wa kujiendesha kwa mapato yake kikitumia taarifa za kidigitali za wanachama wake maarufu kama ‘Chadema Digital.’

Awali, Chadema walitangaza kutumia mfumo huo Desemba 2019 wakati wa Mkutano mkuu uliofanyika jijini Dar es Salaam, lakini haukutekelezwa.

Akizungumza hivi karibuni jijini Arusha ambako Chadema Digital imezinduliwa rasmi katika kanda ya Kaskazini, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe alisema wanakusudia kuandikisha upya wanachama wake kupitia mfumo huo ambapo pia watakuwa wakichangia ada za uanachama.

“Jimbo la Arusha Mjini lina wapiga kura 374,281 ambao tuna uhakika zaidi ya nusu ni watu wetu. Lakini wanachama wetu hawa wanajiona wanyonge kwa sababu hatujaweka mfumo wa kushikamana. Kuanzia leo tunapita kata zote 25, nyumba kwa nyumba kanisa kwa msikiti,” alisema.

“Katika watu 374,000 wa jimbo la Arusha kwa mwezi huu tumeweka lengo tunataka tufikie asilimia 15 sawa na wapiga kura 56,138, ambapo chama chetu kitakusanya Sh140.37 milioni,” aliongeza.

Alisema wameweka lengo la kukusanya zaidi ya Sh561.46 milioni kwa kufikia asilimia 60 ya wanachama wa jimbo la Arusha peke yake ifikapo mwaka 2024 na majimbo mengine.

Katika jimbo hilo pia alisema wamezindua ujenzi wa makao makuu Kanda ya Kaskazini ambapo kutakuwa na ofisi tatu ndani yake, ikiwemo ofisi ya kanda, ya mkoa na ya jimbo.

“Kutakuwa na duka kubwa la kuuza nyaraka za chama, vifaa vya chama na kutakuwa na ukumbi wa kufanya mikutano na mgahawa,” alisema.

Alisema kampeni hiyo itakuwa ni ya nchi nzima, ambapo baada ya kutoka Arusha watakwenda mkoani Shinyanga na mikoa mingine.

Katika ulipiaji wa kadi hizo alisema hazitabagua wanachama wake, kwani wote watakuwa na haki za kugombea na kupiga kura.

Kuhusu matumizi ya fedha wanazokusanya, Mbowe alisema wanakusudia kujenga ofisi za makao makuu ya majimbo na makao makuu ya Taifa.

“Tuliweka msisitizo wa kujenga chama kwenye roho na nyoyo ya watu. Sasa tumesema kabla ya uchaguzi ujao, chama kitajenga makao makuu ya kila kanda Tanzania nzima,” alisema.

Pia alisema wataanzisha chuo cha mafunzo ya itikadi kitakachojulikana kama Edwin Mtei Leadership Academy.

Kwa upande mwingine, Mbowe amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuweka usawa katika ushindani wa vyama vya siasa.

Alisema chama hicho hakitashiriki uchaguzi wowote hadi Katiba mpya iundwe ili kila mmoja aweze kula keki ya Taifa na kuishi kama ndugu.

“Tunawapa nafasi ya kujitafakari tume ya uchaguzi, kwani waliona uonevu wa viwango kwa miaka mitano iliyopita,” alisema Mbowe.

Akirejea mifano ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, Mbowe alisema hawatakubali kuibiwa kwenye chaguzi zijazo.

“Miaka mitano ya awamu iliyopita imeminya demokrasia ya nchi yetu na ilidhihirika katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 na uchaguzi mkuu wa 2020,” alisema.

“Tunataka katiba mpya itakayorekebisha uhuru wa vyama vya siasa kabla ya uchaguzi 2024 na 2025,” alisema.

Imeandikwa na Elias Msuya na Teddy Kilanga,
[email protected]