Chadema: Serikali iweke wazi kushuka bei ya mbolea soko la dunia

Mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo Uvuvi na Mifugo katika Bunge la Wananchi Chadema Pascal Haonga
Songwe. Serikali imetakiwa kuweka wazi kuwa bei ya mbolea kwenye soko la Dunia imeshuka mwaka huu, badala ya kuwadanganya wananchi kuwa inatoa ruzuku wakati haiko katika bajeti ya mwaka huu iliyowasilishwa Bungeni.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo Uvuvi na Mifugo katika Bunge la Wananchi Chadema Pascal Haonga, wakati akizungumza kwenye kikao na waandishi wa habari ofisini kwake.
Haonga anaitaka Serikali iweke wazi kuhusu kushuka kwa bei ya mbolea katika soko la Dunia na si kudai kuwa itatoa ruzuku kwa vile bei inayotangazwa kuwa na ruzuku ni zaidi ya bei halisi iliyopo.
"Taarifa zilizopo bei ya mbolea aina ya UREA inchini Brazil imeshuka kutoka Dola 1400 April mwaka jana hadi kuwa Dola 290 mwaka huu kwa tani, sawa na Sh.34,075 kwa mfuko wa kilo 50 ambapo ukijumlisha na gharama za bandarini na usafiri inatakiwa imfikie mkulima kwa Sh.60,000 kwa mfuko huo," amesema Haonga
Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa bei ya mbolea ya kupandia aina ya DAP inatakiwa imfikie mkulima kwa Sh66, 700 kwa mfuko wa kilo 50 na kuwa bei inayotolewa kama ruzuku ya Sh. 70,000 kwa mfuko huo bado ni kubwa ukilinganisha na uhalisia uliopo.
Aidha Haonga ameitaka Serikali kueleza jinsi itakavyokabiliana na changamoto zilizojitokeza msimu uliopita ikiwemo mawakala kukosekana vijijini, utoroshaji wa mbolea nje ya nchi na changamoto nyinginezo Ili kuboresha huduma na kuhakikisha mkulima anapata pembejeo kwa wakati.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti Tanzania (TFRA) Dk Stephani Ngailo amesema bei zilianza kushuka mwezi Januari na February, ambapo
"Kufuatia hilo Mwezi Machi tukashusha bei na iwapo zikiendelea kushuka tutashusha pia, hapa cha kuelewa ni kuwa inachukua kati ya siku 60-90 mabadiliko ya bei kuwa reflected (kuendana) kwetu," amesema Dk Ngailo.
Mmoja wa wakulima Ismail Ntengwi amesema bei ya mbolea kabla ya kuwekewa ruzuku ilikuwa Sh.120, 000 kwa mfuko mmoja wa kilo 50, lakini baada ya ruzuku ilishuka hadi kufikia Sh.70, 000 ambayo imewawezesha kuzalisha Chakula cha kutosha mwaka huu.
"Zipo changamoto chache ambazo Serikali inahitaji kizifanyia kazi ikiwemo kuongeza idadi ya mawakala hadi vijijini, kudhibiti uvujaji wa mbolea zilizopelekwa nje ya nchi na kuwahisha kabla ya msimu wa Kilimo kuanza," amesema Ntengwi.