Chadema waanza mchakato kuwatoa gerezani Halima Mdee, Matiko na Bulaya

Muktasari:

  • Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kimeanza mchakato wa kuwatoa gerezani mbunge wa Kawe, Halima Mdee; Esther Matiko (Tarime Mjini) na Ester Bulaya (Bunda).

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kimeanza mchakato wa kuwatoa gerezani mbunge wa Kawe, Halima Mdee; Esther Matiko (Tarime Mjini) na Ester Bulaya (Bunda).

Akizungumza na Mwananchi mkurugenzi wa itikadi, uenezi, mawasiliano na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema amesema mawakili wa chama hicho wameanza kufuatilia namba ili kulipa faini ya Sh110 milioni inayotakiwa kulipwa na wabunge hao watatu ili watoke gerezani.

Viongozi wanane wa Chadema pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji jana Jumanne Machi 10, 2020 walihukumiwa kulipa faini ya Sh350 milioni au kwenda jela miezi mitano baada ya kutiwa hatiani kwa makosa 12 kati ya 13 yaliyokuwa yanawakabili.

 

Washtakiwa hao wakiongozwa na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe walilazimika kwenda jela baada ya kushindwa kukamilisha taratibu za kulipa faini hiyo waliyohukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Baada ya hukumu hiyo iliyosomwa  na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, Chadema walianza kuchangishana fedha kwa ajili ya kuwalipia faini viongozi wake hao.

“Hadi leo saa 4 asubuhi tulikuwa tumepata Sh136 milioni, ila tunaanza kulipa Sh110 milioni ili Mdee, Bulaya na Matiko watoke,” amesema Mrema.

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Ziwa, Ezekia Wenje amesema, “kuna mhasibu amekwenda benki kuangalia kiasi kilichoingia. Mchakato wa kuwatoa wafungwa hawa wa kisiasa utaanza leo. Kwa fedha hizi zilizopatikana zinatosha kutoa watu wanne, kwa hiyo tutafanya kwa kadiri wanachama wanavyochanga.”