Chadema washangaa aliyekaa rumande siku 163 kuapishwa ubunge Viti Maalum

Chadema washangaa aliyekaa rumande siku 163 kuapishwa ubunge Viti Maalum

Muktasari:

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kimeshangazwa katibu wa Baraza la Vijana la chama hicho (Bavicha), Nusrat Hanje aliyekaa rumande siku 163  kuapishwa kuwa mbunge wa Viti Maalum siku moja baada ya kuachiwa na polisi.

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kimeshangazwa katibu wa Baraza la Vijana la chama hicho (Bavicha), Nusrat Hanje aliyekaa rumande siku 163  kuapishwa kuwa mbunge wa Viti Maalum siku moja baada ya kuachiwa na polisi.

 Akizungumza leo Jumatano Novemba 25, 2020 katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika amesema kitendo hicho ni mfano hai na ushahidi wa kwanza kuwa kuna mchakato ambao hauihusu Chadema uliotumika ‘kuwateua’ wanachama wao 19 ambao jana waliapishwa kuwa wabunge wa viti maalum bila ridhaa ya chama hicho.

Mnyika amesema ushahidi mwingine ni namna ambavyo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekiuka  masharti ya kikatiba na kisheria yanayosema kuwa kabla ya kufanya uteuzi wa wabunge hao lazima iwe imepata  fomu namba 8D zenye sahihi ya katibu mkuu wa chama husika.

“Mfano Nusrat ambaye amesota mahabusu siku 163 leo Novemba 25 mahakama ndiyo ilikuwa inakutana kutoa maamuzi juu ya rufaa ambayo amekata baada ya kusota ndani muda mrefu,” amesema Mnyika akihoji kutolewa kwa mwanachama huyo na aliyempeleka kuapishwa.

Amesema, “sasa kule bungeni wanasema majina yamepelekwa  Novemba 20 wakati NEC, katiba (ya Tanzania) na  sheria zinasema kabla ya tume kuteua inakuwa na orodha ya fomu za mwombaji, sasa Nusrat alitoka mahabusu Novemba 23 fomu yake alijaza lini?”