Chadema yadai kada wake anashikiliwa na Polisi Zanzibar

Sunday October 03 2021
Chadema pc
By Bakari Kiango
By Jesse Mikofu

Dar/Unguja. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimedai kuwa Mwenyekiti wake wa Baraza la Wazee la chama hicho (Bazecha), anashikiliwa na jeshi la polisi Mjini Unguja.

Hata hivyo akizungumza kwa simu leo Oktoba 3, Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Omar Nassir amesema hana taarifa za kukamatwa mwenyekiti huyo, lakini aliahidi kiongozi huyo lakini akasema anaanza kufuatilia kwenye vituo mbalimbali vya polisi.

"Ungenisaidia kujua sehemu alipokamatiwa, je watu gani waliomkamata kama ni polisi au watu wa kawaida na walikuwa wapoje, hii ingenirahisishia pa kuanzia. Lakini ngoja nianze kuuliza kwenye vituo kisha nitakwambia," amesema Kamanda Nassir.

Akizungumza na gazeti hili leo, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje, John Mrema amesema wamepata taarifa za kukamatwa kwa mwenyekiti wa baraza hilo la wazee na watu waliokwenda nyumbani kwake Unguja.

“Tumepokea hiyo taarifa ya kukamatwa nyumbani kwake Zanzibar na watu waliojitambulisha kuwa askari wa jeshi la polisi.Tunafuatilia kujua amepelekwa kituo gani cha polisi, kisha tutatoa taarifa kamili,” amesema Mrema.

Katika ukurasa wake wa Twitter, Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika aliandika, “Mzee Hashim Issa Juma amechukuliwa nyumbani kwake Zanzibar na watu wasiokuwa na sare waliojitambulisha kwa familia yake kuwa ni polisi. Hawakutaka kusema anapelekwa wapi na sababu za kumchukua.”

Advertisement
Advertisement