Chadema yafanya mazungumzo na Jaji Mutungi kimyakimya
Muktasari:
- Viongozi Wakuu wa Chadema leo wamekutana na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kwa ajili ya masuala mbalimbali ikiwemo kuimarisha hali ya kisiasa hasa demokrasia vya vyama vingi.
Dar es Salaam. Viongozi Wakuu wa Chadema leo wamekutana na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kwa ajili ya masuala mbalimbali ikiwemo kuimarisha hali ya kisiasa hasa demokrasia vya vyama vingi.
Kikao hicho kimefanyika leo Alhamisi Agosti 24, 2023 katika ofisi ndogo za msajili zilizopo Posta Jijini Dar es Salaam.
Kikao hicho, Chadema iliwakilishwa na mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, John Mnyika, na Katibu wa Baraza la Wazee la Chadema (Bazecha), Rodrick Rutembeka, huku Ofisi ya Msajili iliwakilishwa Jaji Mutungi, Naibu Msajili msaidizi, Sisty Nyahoza, Naibu Msajili, Mohamed Ali Ahmed na Mkuu wa Kitengo cha Sheria Muhidin Mapeyo.
Baada ya kikao hicho zilizasambwa picha katika mitandao ya kijamii zikiwaonyesha viongozi hao kutoka Chadema na Ofisi ya Msajili, wakiwa pamoja.
Hata hivyo, hakukuwa na taarifa zaidi zikieleza kilichozungumziwa kwa undani kati ya viongozi wa taasisi hizo.
Mwananchi Digitali lilimtafuta Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itikadi, Uenezi na Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mrema, aliyejibu kwa kifupi akisema ni kikao cha kawaida.
“Nipo Geita, ninachojua ni kikao cha kawaida kati Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na viongozi wa vyama vya siasa,” amesema Mrema.