Chadema yagongelea msumari mwingine sakata la kina Mdee

Katibu wa Chadema Kanda ya Kati, Emmanuel Masonga. Picha na Habel Chidawali

Muktasari:

Katibu wa Chadema Kanda ya kati, Emmanuel Masonga amesema wamepeleka barua ya kutowatambua wabunge 19 kwa Spika wa Bunge.

Dodoma. Kwa mara nyingine Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) leo kimekabidhi barua kwa Spika wa Bunge la Muungano wa Tanzania, Dk Tulia Ackson kumtaarifu kuwa wabunge 19 wa viti maalumu waliopo bungeni kwa mgongo wa chama hicho,  siyo wanachama halali.

Hii ni mara ya pili kwa Chadema kupeleka barua kwa Spika kueleza kuwa wabunge akiwamo Halima Mdee na wenzake 18, si wanachama wao na kutaka uongozi wa Bunge kuwatimua.

Mdee na wenzake 18 waliingia kwenye mgogoro na chama chao baada ya kuelezwa kuwa walijipeleka kuapishwa bila ridhaa ya uongozi wa Chadema.

Leo Jumatatu Desemba 18, 2023, Katibu wa Kanda ya Kati, Emmanuel Masonga amekiri kufikisha barua hiyo kwa Spika ambapo imepokelewa na wasaidizi wake.

Mbali ya kupeleka bungeni, nakala ya barua hiyo imepelekwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa na Ikulu ya Chamwino.

"Maeneo yote nimepokelewa vizuri isipokuwa kwa Spika ambapo kulitokea changamoto kidogo kwamba wasaidizi wake walitaka kugoma, lakini baada ya wao kuwasiliana na kiongozi huyo aliwaagiza wapokee nikawapatia," amesema Masonga.

Katibu huyo amesema kilichotokea ofisi ya Spika ni kitu cha kawaida, kwani umakini unatakiwa kwa wasaidizi wa kiongozi mkubwa kama Spika.

Hata hivyo, amesema hajui kinachoendelea kwani baada ya hapo kazi iliyobaki ni ya makao makuu ya Chadema kuendelea na ufuatiliaji, huku yeye akisubiri maelekezo kutoka kwa wakubwa wake.

Pia amewaomba wanachama kuwa watulivu na waendelee kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za mitaa hivyo waendelee kujiandikisha kwenye mfumo wa digitali.

Wiki iliyopita Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ilitoa uamuzi wa kufuta uamuzi wa Baraza Kuu la Chadema dhidi ya waliokuwa wanachama wake 19 wa kuwafukuza uanachama.

Hatua hiyo ilipokelewa kwa faraja na Mdee ambaye juzi, aliliambia Mwananchi kuwa hali hiyo inaonyesha matumaini kuhusu kumalizika kwa mgogoro huo.

Lakini, uamuzi huo wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ni kama vile umekoleza joto ndani ya Chadema ambao wameibuka upya na kuendelea kuandika barua za kutowatambua wabunge hao.