Chadema yawapa kongole Polisi Mwanza

Maofisa wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza wakipanga na kuongoza magari wakati viongozi wa kitaifa wa Chadema walipokuwa wakijiandaa kuanza msafara wa kwenda eneo la Buhongwa kwa ajili ya mapokezi rasmi kabla ya kwenda viwanja vya Furahisha jijini Mwanza unakofanyika mkutano wa uzinduzi wa mikutano ya hadhara ya chama hicho. Picha na Mpigapicha Wetu.

Muktasari:

  • Chadema wanafanya mkutano wa kwanza wa hadhara baada ya takriban miaka saba kutokana na zuio la mikutano ya kisiasa iliyowekwa na Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli mwaka 2016. Zuio hilo limeondolewa karibuni na Rais Samia Suluhu Hassan.

Mwanza. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeipa kongole Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kwa kukipa ushirikiano kufanikisha mkutano wa hadhara wa chama hicho unaofanyika jijini Mwanza leo.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Januari 21, 2023, Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, Zakaria Obadi amesema chama hicho kimepokea kwa furaha jinsi uongozi wa Jeshi la Polisi Wilaya za Nyamagana na Ilemela mkoani Mwanza ulivyosaidia kufanikisha mkutano huo unaofanyika viwanja vya Furahisha.

"Kusema ukweli tunawapongeza na kuwashukuru Jeshi la Polisi Mwanza; wametoa ushirikiano unaostahili kwa mujibu wa sheria ikiwemo kuwapokea na kuwapa ukinzi viongozi wetu wa kitaifa wakiongozwa na Mwenyekiti wetu Freeman Mbowe," amesema Obadi

Ameongeza; "Tunaamini viongozi wa Jeshi la Polisi katika mikoa mingine wataiga mfano bora ulioonyeshwa na wenzao wa Mwanza kwa kutimiza wajibu na jukumu la ulinzi na usalama katika mikutano na shughuli za kisasa za vyama vyote kwa haki na usawa kwa mujibu wa sheria,"

Chadema yakiwasha Mwanza, Mbowe achukizwa 'kulamba asali'

Jeshi la Polisi limeimarisha ulinzi kuanzia katika hoteli la kitalii iliyoko katikati ya jiji la Mwanza walikofikia viongozi wa kitaifa na makada wa Chadema.

Pamoja na ulinzi hotelini, askari polisi wakiwa katika magari matatu wameonekana wakiimarisha ulinzi katika msafara wa viongozi wa Chadema wakiongozwa na Mbowe uliokuwa ukielekea eneo la Buhongwa, nje kidogo la jiji la Mwanza yanakofanyika mapokezi rasmi kabla ya kwenda viwanja vya Furahisha kuhutubia mkutano wa hadhara.

Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika ameiambia Mwananchi kuwa pamoja uzinduzi wa mikutano mingine itayaofanyika maeneo mbalinbali nchini, mkutano wa leo pia ni sehemu ya kumbukizi ya miaka 30 tangu Chadema iliposajiliwa rasmi mwaka 1993.