Chalamila atishia kumweka ndani mkandarasi mwendokasi

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema mkandarasi amekuwa akijinasibu kufanya kazi usiku na mchana lakini hakuwahi kumshuhudia

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema haridhishwi na kasi ya ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka ya Gongo la Mboto.

Amesema kama hali itaendelea hivyo, atamweka ndani mkandarasi au mhandisi mshauri.

Ametoa kauli hiyo leo Aprili 18, 2024 alipofanya ziara kukagua ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 23.6 kutoka Gongo la Mboto hadi katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

Ujenzi huyo unaotekelezwa na Mkandarasi Syno Hydro ni awamu ya tatu ya mradi wa mabasi yaendayo haraka.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila akizungumza na wananchi wakati akifanya ukaguzi wa ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka ya awamu ya tatu yenye urefu wa Km23.6

Chalamila amefanya ziara baada ya kuwapo malalamiko kutoka kwa wakazi wa eneo hilo juu ya tabu wanayopata kutokana na ubovu wa barabara uliosababishwa na ujenzi unaoendelea.

Amesema mara zote mkandarasi amekuwa akijinasibu kufanya kazi usiku na mchana lakini hakuwahi kumshuhudia.

Chalamila amesema amethibitisha hilo kupitia ziara za kushtukiza katika eneo hilo alizofanya usiku kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo.

“Makandarasi mliopewa jukumu hili muda si mrefu naweza nikawatia ndani kwa sababu kasi ya ujenzi hairidhishi kila siku mnajitetea mvua, kama unajua mvua si uamke asubuhi na mapema ufanye kazi mpaka usiku kwa sababu kesho kutakuwa na mvu,” amesema.

Chalamila amewataka kujipanga ndani ya siku chache kwa sababu njia ya Gongo la Mboto ina watu wengi, hivyo kama mkandarasi ataendelea na hali aliyonayo atakinyima kura chama tawala.

“Barabara ni chafu kwa sababu watu wanafanya kazi saa 11 jioni wanaenda kulala na Dar es Salaam tunataka kazi saa 24, nimekuja kuwaambia sijaridhishwa, sasa nikishindwa kumkamata mkandarasi nitakamata msimamizi aliye sehemu yoyote hata Tanroads,” amesema Chalamila.

Mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo ulisainiwa Machi 17, 2022 na ulipaswa kuanza Agosti Mosi mwaka huo, huku miezi 20 ikitarajiwa kutumika itakayoisha Agosti, 2024.

“Nikiangalia kwa kasi hii bado watakuwa hawajamaliza, huku Gongo la Mboto kuna matatizo mengi, maeneo ambayo barabara zimeharibika pengine kuliko mahali popote huenda ni huku, sasa wahangaishwe kwenye treni, wahangaishwe kwenye mwendokasi, wahangaike sijui Kivule barabara zimekufa hapa hii hatuwezi,” amesema Chalamila.

Amemtaka Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Dar es Salaam kwenda kujipanga kuhakikisha kazi inafanyika usiku na mchana.

Amemtaka meneja huyo kuainisha mipaka ya barabara ili utaratibu wa kupanda miti na bustani uanze sambamba na maeneo ya abiria kupumzika.

Amesema kutokana na hilo, amewaita watendaji wa mitaa ambao maeneo yao yanagusa barabara kuu kwa ajili ya kikao ili wawaeleze wananchi kuwa lazima maeneo hayo yapendeze.

Akizungumzia usafi, Chalamila amesema Gongo la Mboto ni moja ya maeneo yasiyo safi, akishangaa kuwa mpaka sasa hakuna kipindupindu.

Amemtaka mkandarasi aliyeshinda zabuni ya kufanya usafi eneo hilo kuongeza kasi.

Pia, amemuagiza mkuu wa wilaya kumuangalia ikiwa hafanyi kazi vizuri aondolewe.

“Nampatia wiki mbili, asipobadilika namfukuza kazi na hatapata kazi tena katika Mkoa wa Dar es Salaam. Jamani mnakijua kipindupindu, kikiingia katika mji huu ni hatari, hakuna mtalii atakuja wala shule kufunguliwa kwa sababu ugonjwa huu ni mbaya na kipindupindu maana yake ni kula kinyesi kibichi,” amesema.

Chalamila amewataka wananchi kuzingatia usafi akieleza kwa hadhi ya jiji hili si la kuanza kutoa elimu ya usafi.

Awali, akisoma taarifa ya utekelezaji, msimamizi wa mradi huo kutoka Tanroads, Frank Mbilinyi amesema ujenzi umefikia asilimia 45.6.

“Malengo yetu hadi Desemba mwaka huu barabara zote ziwe zimekamilika na zibaki kazi nyingine ndogo-ndogo ambazo zitafanyiwa kazi Machi 2025,” amesema.

Mbilinyi amesema mvua zinazoendelea kunyesha ni sababu ya mradi kutofanyika kwa kasi kubwa licha ya mkandarasi kufanya kazi usiku na mchana.

Lawrence Mlimwa, mmoja wa wakazi wa Gongo la Mboto ameiomba Serikali kuingilia kati ili ujenzi wa barabara hiyo uharakishwe.

“Wanajenga kwa ajili ya maendelo yetu lakini tabu tunayoipata ni kubwa. Barabara zimekuwa mbovu, mvua ikinyesha hakupitiki, ukisema upande bodaboda labda uwe umebeba nguo za ziada maana unaweza kumwagiwa tope ukashindwa kuingia hata ofisini,” amesema Mlimwa.

Amesema hali hiyo imefanya usafirishaji kuwa mgumu jambo linaloongeza muda wanaotumia barabarani.

“Tutapata sonona maana tunatumia muda mwingi njiani, foleni, maudhi, wakati mwingine unapata msongo wa mawazo kwa sababu unaona kabisa ukichelewa kazini japo umewahi kuamka,” amesema Mlimwa.