Nusu ya barabara za Dar ni mbovu, kilio chatanda

Dar es Salaam. Unapoingia jijini Dar es Salaam kupitia Barabara ya Morogoro, utapokewa na barabara za kuvutia zenye madaraja ya juu yanayopita magari na ya waendao kwa miguu, hakika utaona sura ya jiji inayopendeza.

Lakini unapoanza kuingia mitaani, utachoshwa na barabara mbovu na kwa kipindi hiki cha mvua, nyingi zimejaa maji katika mahandaki na kutengeneza madimbwi, huku nyingine zikishindwa kupitika kabisa.

Mwananchi imezungumza na baadhi ya wananchi, walioeleza kuchoshwa na kero za barabara hizo, licha ya ahadi za kila mwaka za wanasiasa kuzijenga.
 

Malalamiko ya wananchi

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mbondole, Thomas Nyanduli alisema barabara hiyo ina mashimo makubwa yaliyojaa maji na kusababisha magari kushindwa kupita.
Alisema Serikali ilishapanga bajeti mwaka jana na mkandarasi alishapatikana tangu Septemba mwaka 2022 na kwa mujibu wa meneja wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tarura) jiji la Ilala aliwaeleza kuwa barabara hiyo ilitakiwa kujengwa kwa kiwango cha changarawe.

“Januari mwaka huu tulimuona mkandarasi akileta vifaa, alikaa mwezi mmoja akamwaga vifusi kwenye mashimo machache, kisha akaondoka, hakuna kilichoendelea, matokeo yake mvua zilipoanza maji yamejaa kwenye mashimo,” alisema Nyanduli.

Kwa upande wa mkazi wa Kivule, Laurent Kivuyo alisema wameipazia sauti kwa muda mrefu barabara yao inayoelekea Hospitali ya Wilaya ya Ilala, kwani ina madimbwi ya maji.

“Hii barabara ilitakiwa ipewe kipaumbele, ijengwe kutokana na umuhimu wake maana inabeba uhai wa watu wengi,” alisema Kivuyo.

Magdalena Juma ni mkazi wa Kimara Golani, naye alilalamikia ubovu wa barabara unaosababisha usafiri wanaotumia wa pikipiki kupanda bei. “Usafiri wa bajaji ulikuwa Sh700 kwa zile za kuchangia na pikipiki ilikuwa Sh1,500, lakini kutokana na ubovu wa barabara hiyo nauli imepanda hadi kufikia Sh1,000 kwa bajaji na Sh2,000 kwa pikipiki.

Pia ni hatari, kwani huwa tunapata ajali mara kwa mara kutokana na kukithiri kwa mashimo katika barabara hii,” alisema.
 

Asilimia 50 ya barabara ni mbovu

Wakati baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam, wakilalamikia ubovu wa barabara nyingi za mitaa, Meneja wa Tarura mkoani humo, Geofrey Mkinga alisema asilimia 50 ya mtandao wa barabara za ndani kwa jiji hilo ni mbovu na wanahitaji Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP), kupata suluhu.

Alisema asilimia 11 ya mtandao huo una hali nzuri na asilimia 39 una hali nzuri ya wastani. Alisema Serikali imeshaanza mazungumzo ya kuleta mradi wa DMDP ili kutatua tatizo hilo.

“Hakuna nchi duniani imekua kwa mwaka mmoja au kwa miaka miwili, tunaanza kutatua zile zenye changamoto na zinazohudumia watu wengi ndiyo zitaletewa mradi wa kimkakati kama DMDP,” alisema.

Alifafanua kuwa barabara zitakazonufaika na mradi wa DMDP ni Banana, Kivule, Pugu Majohe hadi Pondole, Barabara ya Moshi Bar ambazo zina kelele nyingi na nyingine maeneo ya Kigamboni, Temeke, Mbezi Msumi, Suka Golani na Salasala Mbezi.

Mkinga alisema mpango wa DMDP unaweza kuja kutatua na kupata suluhu kwa kujenga barabara mbovu zote na zinazolalamikiwa kwa kiwango cha lami na changarawe kwa awamu, kurahisisha usafiri kwenye maeneo hayo yanayohudumia watu wengi.

Alisema hata mkataba uliosainiwa juzi na Halmashauri ya Jiji hilo wenye thamani ya Sh5.8 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa barabara nane za mitaa kwa kiwango cha lami na zege na daraja moja lililopo katika Barabara ya Kifaru Majoka, ni mipango ya muda mfupi. “Pamoja na kuanza mchakato wa mpango mkubwa hatuwezi kuacha kuja na mpango wa muda mfupi na muda wa kati, Dar es Salaam ina watu na magari mengi, tunahitaji kufanya usanifu kwa pamoja, zinahitajika taa na njia za watembea kwa miguu ili kuwa na usalama,” alisema Mkinga.
 

Mkataba Sh5.8 bilioni wasainiwa

Katika hafla ya utiaji saini mikataba ya kujenga baadhi ya barabara za Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa jiji hilo, Mhandisi Amani Mafuru alisema fedha hizo zimetengwa kutokana na mapato ya ndani na zinaenda kujenga barabara katika majimbo matatu ya Ukonga, Segerea na Ilala.

“Tumejitahidi kupata makandarasi wazuri wanaoweza kukamilisha kazi hii ndani ya kipindi cha miezi sita kupata barabara nzuri ili kurahisisha usafiri,” alisema.

Alisema barabara zinazoenda kujengwa ni Pugu Majohe yenye urefu wa kilomita 0.4, Kitunda-Kivule-Msongola yenye urefu wa kilomita 0.5, Kwampalange-Mwanagati-Kitunda urefu kilomita 0.5 na zote kwa jumla zikiwa na kilomita 1.4 na zitajengwa na mkandarasi Southern Link kwa thamani ya Sh1.9 bilioni.
“Barabara nyingine ni Nyati km (0.38), Rufiji yenye urefu wa kilometa 0.36, Mchikichini kilomita 0.35 zote kwa kiwango cha lami, huku zitakazojengwa kwa kiwango cha zege zikiwa ni Barabara ya Mtendeni kilomita 0.78 na Southern kilomita 0.1 zote zikiwa na thamani ya Sh1.9 bilioni zitakazojengwa na mkandarasi EMJS Construction,” alisema Mafuru. Alisema usimamizi wa ujenzi huo utakuwa chini ya Tarura, ambao wana jukumu la kufanya usanifu.
 

Latra watangaza ruti mpya

Wakati Tarura wakikiri ubovu wa miundombinu hiyo, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), Aprili 11 mwaka huu ilitangaza njia mpya zitakazopita usafiri wa umma maarufu kama daladala zikihitaji magari 220. Ilitoa vigezo vya wanaotakiwa kuomba kutoa huduma katika njia hizo, ikiwamo kuwa na magari yenye uwezo wa kubeba abiria kuanzia 15 na 25.

Mkurugenzi wa Latra, Johansen Kahatano alisema, “Mtu anapotaka njia tunaipima kwanza baada ya kupokea maombi kutoka kwa wananchi, pia tunafanya utafiti wenyewe wa kupitia kuona kama inaweza kutumika na kuunganika na nyingine,” alisema Kahatano.

Imeandaliwa na Tuzo Mapunda, Nasra Abdallah, Fortune Francis na Mariamu Mbwana