Chalamila awatangazia neema wanawake Dar
Mkuu wa Mkoa wa Dar ea Salaam, Albert Chalamila, akimkabidhi cheti cha utunzaji wa mazingira, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Kampuni ya Suma- JKT, Kapteni Rosemary Katani katika maadhimisho ya siku ya mazingira duniani leo Juni 5, 2024.
Muktasari:
- Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amewataka madiwani wanawake na wakuu wa wilaya tano za mkoa huo, kuandaa orodha ya kina mama wenye kipato cha chini kwa ajili ya kupewa mitungi ya gesi.
Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar ea Salaam, Albert Chalamila ametoa ofa ya mitungi ya gesi 1,500 kwa kina mama kutoka wilaya za tano za Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya uhamasishaji wa nishati safi ya kupitia na kuondokana na matumizi ya kuni na mkaa.
Chalamila ametoa ofa hiyo leo Jumatano Juni 5, 2024 wakati maadhimisho ya siku ya mazingira duniani yaliyofanyika uwanja wa Mji Mwema wilayani Kigamboni kwa mkoa wa Dar es Salaam.
Juni 5 ya kila mwaka, Tanzania inaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku ya mazingira duniani ambapo kwa mwaka huu yana kauli mbiu ya urejeshwaji wa ubora wa ardhi, kukabiliana na hali ya jangwa na ustahimilivu wa ukame.
"Muda si mrefu mkuu wa wilaya (ya Kigamboni -Halima Bulembo) nitaomba unipatie orodha ya kinamama 300 wanaotoka katika mazingira yenye kipato kidogo.Hii ofa niitoe pia kwa madiwani wa viti maalumu na kata za wilaya tano.
"Katika kata zenu nitahitaji angalau wanawake 300 kutoka kila wilaya ambao ofisi ya mkuu wa mkoa itawawezesha kuwapata mitungi ya gesi kwa matumizi bora ya nishati safi," amesema Chalamila.
Amesema hayo yote kuunga mkono safari aliyoianzisha Rais Samia Suluhu Hassan kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuondokana na nishati chafu zinazoleta madhara kwa binadamu ikiwemo kusababisha magonjwa ya upumuaji.
" Wengi wanahisi Rais Samia anawaumiza Watanzania anapotaka watumie gesi, lakini ukweli usiopingika Rais anajali afya za wananchi kwa sababu matumizi ya mkaa yana madhara kwa binadamu.
"Tulichukulie jambo hili kwa mtazamo mzuri kwa Rais Samia anajali afya za wananchi kwa manufaa ya kizazi cha leo na kesho, kwa maslahi mapana na endelevu ya Taifa letu," amesema Chalamila.
Mbali na hilo, Chalamila amewataka wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo, kuhakikisha wanachukulia hatua za kisheria watu watakaobainika kutiririsha majitaka.
"Lakini pia nitoe rai mnaweza kuwatafuta vijana watakaokuwa na jukumu kuelimisha na kukamata watu wanaotupa taka ovyo kisha kuwapiga faini ambayo asilimia 30 itabaki kwao na asilimia 70 inakwenda halmashauri," amesema Chalamila.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Halima Bulembo, amesema wamekuwa wakitekeleza kwa vitendo suala la utunzaji wa mazingira ikiwemo usafishaji wa fukwe unaofanyika kila mara wilayani humo.
"Mheshimiwa mkuu wa mkoa tumeendelea kutekeleza kwa vitendo maelekezo yako ya kufanya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kwa ushirikiano na wananchi wa Kigamboni," amesema Bulembo.
Katika maadhimisho hayo baadhi ya taasisi za umma na binafsi kutoka wilaya tano za mkoa huo zilipewa tuzo za vinara bora wa kutunza mazingira Dar es Salaam.
Kampuni ya Suma - JKT ilibuka kinara katika utunzaji wa mazingira kwa manispaa ya Ubungo, ambapo mkurugenzi wa uendeshaji taasisi hiyo, kapteni Rosemary Katani ameushukuru uongozi wa mkoa wa Dar ea Salaam kwa kutambua jitihada zao katika usafi.
" Mwaka jana tulibuka vinara katika manispaa ya Kinondoni, mwaka huu tumepata Ubungo, siri ya mafanikio ni kuwa na vifaa vya kisasa na kujituma kwa ufanisi katika shughuli zetu," amesema Kapteni Katani.