Chanzo cha samaki kufa mto Mara chatajwa

Mkurugenzi wa bodi ya maji Bonde la Ziwa victoria, Renatus Shinhu akitoa ripoti ya awali ya utafiti uliofanywa kuhusu maji ya mto Mara kuchafuka na kubadilika rangi kuwa nyeusi jambo lililopelekea samaki kufa ndani ya mto huo. Picha na Mgongo Kaitira.

Muktasari:

  • Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) imeeleza kuwa uchunguzi wa awali wa kimaabara umebaini uwepo wa kiwango kikubwa cha mafuta na kukosekana kwa hewa ya Oksijeni kwenye maji ya mto Mara jambo lililosababisha samaki na viumbemaji kufa.


Mwanza. Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) imeeleza kuwa uchunguzi wa awali wa kimaabara umebaini uwepo wa kiwango kikubwa cha mafuta na kukosekana kwa hewa ya Oksijeni kwenye maji ya mto Mara jambo lililosababisha samaki na viumbemaji kufa.

Machi 8, 2022 vipande vya video vilivyosambaa katika mitandao ya kijamii vilionesha samaki na viumbe wanaoishi ndani ya mto huo katika daraja la Kirumi mkoani Mara wakiwa wamekufa na kuelea jambo lililozua taharuki kwa wakazi na wavuvi wanaoendesha shughuli za uvuvi katika mto huo.

Uchunguzi huo umeanza kufanyika Machi 8, 2022 baada ya bodi hiyo kupokea taarifa ya uwepo wa uchafuzi wa maji uliosababisha maji kuwa meusi na kufa kwa samaki katika mto Mara kwenye eneo la Kirumi Darajani.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 12 jijini Mwanza, Mkurugenzi wa bodi hiyo, Renatus Shinhu ametaja vijiji vilivyoathirika kutokana na uchafuzi huo kuwa ni Kirumi, Kwibuse, Marasibora, Ketasakwa na Ryamisanga.

“Uchunguzi wa kimaabara umeonesha mambo mawili ikiwemo kuwepo kwa kiwango kikubwa cha mafuta kuliko kiwango kinachokubalika kwa mujibu wa viwango vya ubora wa maji Tanzania (TZs 2068:2017),” amesema Shinhu.

Amesema sampuli ya maji iliyochukuliwa Machi 8 mwaka huu ilionyesha kuna kiwango sifuri cha Oksijeni katika eneo la Kirumi huku siku tatu baadae kiwango hicho kikiongezeka na kufikia asilimia mbili ambayo inaelea moja kufikia kiwango cha kawaida kinachohitajika kwa viumbe wanaoishi ndani ya mto huo.

"Kiwango kikubwa cha mafuta kwenye maji ndicho kilichosababisha kuisha kwa hewa ya okisijeni kwenye maji na kuathiri viumbe hai ikiwa ni pamoja na samaki hivyo tunaendelea kufanya utafiti kubaini kwa undani yalipotoka mafuta hayo," amesema.

Wakati LVBWB ikitoa taarifa hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Selemani Jaffo ameunda kamati maalum ya kitaifa itakayofanya uchunguzi wa chanzo cha mabadiliko katika mto Mara yaliyosababisha maji ya mto huo kubadilika rangi na kuwa nyeusi.

Jaffo ametangaza kamati hiyo ya watu 11 leo Machi 12, 2022 mjini Musoma baada ya kufanya ziara ya siku moja kujionea hali halisi katika mto huo huku akikiri kuwa hali si shwari hivyo jitihada za haraka zinatakiwa kuchukuliwa.

Ametoa siku saba kuanzia leo kwa kamati hiyo ambayo iko chini ya mwenyekiti wake, Mhandisi katika Idara ya Kemia na Madini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Samuel Mayere.

Ametaja wajumbe wengine kuwa ni katibu wa kamati hiyo ambaye ni Mkurugenzi wa Mkuu wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (Nemc), Dk Samuel Gwamaka na wajumbe wengine wakiwa ni Dk Charles Kasanzu kutika idara ya jiolojia chuo kikuu cha Dar es salaam.

Pia kuna Mkurugenzi wa Udhibiti Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Daniel Nio, Mkurugenzi wa bodi ya maji bonde la ziwa Victoria,  Renatus Shinu, Mkurugenzi wa taasisi ya Utafiti wa Samaki (Tafiri) kanda ya ziwa, Baraka Sekadende na mjumbe mmoja kutoka Ofisi ya Rais.