Chanzo kifo cha Jengua

Chanzo kifo cha Jengua

Muktasari:

Maua Ally  ambaye ni mke wa mwigizaji wa filamu na tamthilia nchini Tanzania, Mohamed Fungafunga maarufu Jengua amesema mumewe alikuwa akisumbuliwa na presha.

Dar es Salaam. Maua Ally  ambaye ni mke wa mwigizaji

wa filamu na tamthilia nchini Tanzania, Mohamed Fungafunga maarufu Jengua amesema mumewe alikuwa akisumbuliwa na presha.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne Desemba 15, 2020 Maua amesema amefariki wilayani Mkuranga, nyumbani mwa mwanaye mkubwa aliyekuwa akimuuguza.

“Alikuwa anasumbuliwa na presha kwa hiyo tulikuwa Mkuranga kwa mtoto wake mkubwa kwa ajili ya kumuuguza lakini leo tumeamka asubuhi hali ikawa mbaya na amefariki hapa nyumbani,” amesema  Maua na kubainisha kuwa mazishi yatafanyika kesho  saa saba mchana jijini Dar es Salaam katika makaburi ya Mburahati.

Msemaji wa  chama cha waigizaji Dar es Salaam, Masoud Kaftan amesema, “ tuliona taarifa mitandaoni lakini baada ya kufuatilia na kuthibitisha kuwa ni kweli tumepokea kwa majonzi taarifa za kifo.

Umaarufu wa Jengua ulianza mwanzoni mwa miaka ya 2000 alipoigiza katika tamthilia zilizokuwa zikiandaliwa na kikundi cha Chemchemu Arts Group.

Katika tamthilia hiyo aliigiza kama mzazi asiyethamini watoto wake wa kike na kukataa kuwapeleka shule huku yeye akiwa na uhusiano na wanafunzi.