Chibulunje akemea uuzaji ardhi kiholela

Naibu waziri mstaafu, Hezekiah Chibulunje akizungumza kwenye mkutano wa Mikalile ye Wanyausi. Kushoto ni mwenyekiti wa umoja huo, Grace Lesilwa na Kulia, Kaimu Katibu Gelshom Maloda.

Muktasari:

  • Hezekiah Chibulunje, aliyekuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, amesisitiza umuhimu wa elimu itakayosaidia watu kujitambua na kutouza ardhi kinyemela.

Dodoma. Naibu Waziri wa Ujenzi wa zamani, Hezekiah Chibulunje amewataka wakazi wa Mkoa wa Dodoma kuwa makini na wimbi la kuuza ardhi, kwani halitawaacha salama.

Chibulunje ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Desemba 26, 2023 alipozungumza kwenye mkutano mkuu wa mwaka kundi la Mikalile ye Wanyausi ambao huwakusanya Jamii ya Wagogo.

Amesema uuzaji wa ardhi umekuwa mkubwa na usio na mpangilio ambao husababisha watu kuwa walalamikaji kwa mambo waliyoyafanya.

"Msiuze ardhi bila mpangilio, kila jambo linakwenda kwa utaratibu wake, ingawa ni vizuri mtu kutumia kilicho chake, lakini unauza kwa kufanyia nini?

"Mnapofanya jambo lolote mahali popote msiache kuweka alama mlikotoka, ili watu wa vijiji vyenu watambue umuhimu wa kusomesha watoto kwamba kuna faida," amesema.

Pia amesisitiza umuhimu wa elimu kwa vijana wote wa mjini na vijijini, kwani Serikali imefanya uwekezaji mkubwa wa majengo na vifaa, hivyo lazima watoto wapelekwe shule.

Akizungumzia ugonjwa wa fistula, amesema ni wakati wa kuyaweka wazi matatizo makubwa kama ugonjwa huyo na kila mmoja asimame imara kulisemea.

Chibulunje amekubali kuwa miongoni mwa wazee wa kuwaelimisha watu madhara hayo bila woga, kwa kuwa anaamini ndiyo njia pekee ya kuwasaidia waliopatwa na matatizo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mikalile ye Wanyausi, Grace Lesilwa amesisitiza suala la elimu kwa kila mtoto, ili kuongeza uelewa na kufuta ujinga kwa wakazi wa mikoa ya Dodoma na Singida ambao wanaonekana bado wako nyuma.

Lesilwa amesema moja ya miongoni mwa malengo yao ni kutunza mazingira, kuhamasisha kuhusu elimu, kuibua changamoto zilizopo kwa jamii na kujenga makumbusho, kazi zinazoendelea hadi sasa.

Kwa mujibu wa Lesilwa kwa kipindi cha 2023, Mikalile imetoa madawati 30 kwa shule mbili za msingi Manyoni na kusaidia mmoja wa wanafunzi kusoma chuoni baada ya kubainika wazazi wake hawakuwa na uwezo.

Mjumbe wa kundi hilo, Peter Mavunde ametaka uwepo msingi imara wa kundi hilo kwa ajili ya kuwasaidia wenye uhitaji wa elimu ikiwemo wanaotoka mazingira magumu.

Mavunde amewaomba wanachama wa kundi hilo kujitolea zaidi na kuwekeza nguvu zao kwenye mipango hai, badala ya kusimamia mambo yasiyo na faida kwao na vizazi vyao.