China yaipa JWTZ magari 40, Magufuli atoa pongeza

Muktasari:

  • eshi la Ukombozi la Watu wa China (PLA) limetoa magari 40 kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) huku Rais wa Tanzania, John Magufuli aliyepokea magari hayo akipongeza jeshi hilo na kutoa ombi jingine kwa PLA.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amemshukuru Rais wa China, Xi Jinping kwa kuuendeleza ushirikiano na uhusiano mzuri wa Tanzania na China ikiwemo misaada na uwekezaji ambao China inaufanya  nchini humo.

Rais Magufuli ametoa shukrani hizo leo Alhamisi Septemba 12, 2019 katika hafla ya makabidhiano ya magari 40 kutoka Jeshi la Ukombozi la Watu wa China (PLA) kwenda Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) iliyofanyika Makao Makuu ya JWTZ Upanga Jijini Dar es Salaam.

Magufuli amesema magari hayo 40 yataimarisha utendaji kazi wa jeshi hilo na kuomba PLA isaidie upatikanaji wa ndege kubwa za kubebea askari na vifaa kwa ajili ya jeshi hilo.

Amesema pamoja na kuisaidia Tanzania katika maeneo mbalimbali ya huduma za kijamii, ulinzi na usalama na miundombinu, China ndio nchi inayoongoza kwa uwekezaji hapa Tanzania ikiwa na miradi 723 yenye thamani Sh13.581 trilioni  iliyozalisha ajira 87,126.

Ametaka uhusiano huo uimarishwe zaidi kwa JWTZ na PLA kujenga kiwanda kikubwa chenye uwezo wa kubangua tani laki mbili za korosho kwa mwaka, jambo ambalo litasaidia kuongeza thamani ya korosho za wakulima wa Tanzania na kupelekwa China ambako kuna mahitaji makubwa ya korosho.

“Makabidhiano haya ya magari 40 ni kielelezo kingine tena cha uhusiano wa karibu, kidugu na kirafiki uliopo kati ya mataifa yetu mawili.”

“Tunaishukuru sana China kwa misaada mbalimbali iliyoitoa kwa Tanzania, China imekuwa mdau mkubwa wa biashara kwa nchi yetu na pia inasaidia katika utalii, kwa mfano mwaka huu tunatarajia kupata watalii 10,000 kutoka China,” amesema Rais Magufuli.

Kwa upande wake, Luteni  Jenerali  Yuanming amemshukuru Rais Magufuli kwa kuhudhuria tukio hilo na kwa kuendeleza na kuukuza uhusiano wa Tanzania na China ukiwemo uhusiano wa kijeshi na ameahidi kuwa PLA itaendelea kushirikiana kwa ukaribu na JWTZ.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo ametaja baadhi ya maeneo ambayo JWTZ imenufaika kutokana na ushirikiano wake mzuri na PLA ni pamoja na kujengwa kwa Kituo cha Mafunzo ya Kijeshi huko Mapinga wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani, ukarabati na ujenzi wa uwanja wa ndege wa Ngerengere na ujenzi wa awamu ya pili ya Chuo cha Ulinzi wa Taifa Mkoani Dar es Salaam (NDC) .

Pia, amesema kwa sasa PLA inakamilisha maandalizi ya kujenga Makao Makuu ya JWTZ mkoani Dodoma na kushirikiana na JWTZ katika kazi kubwa la kijeshi litakalofanyika hapa nchini kwa lengo la kubadilishana ujuzi katika ulinzi na usalama.