Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chongolo aeleza upekee wa Monduli akiwataja Sokoine na Lowassa

Waziri wa Kilimo, Godfrey Chongolo ameweka jiwe la msingi la uzinduzi wa Kituo cha Afya Lowassa Sepeko, kilichopo Kijiji cha Mti Mmoja, Kata ya Sepeko wilayani Monduli, Mkoa wa Arusha.

Muktasari:

  • Monduli ni miongoni mwa wilaya sita za Mkoa wa Arusha ambapo kuna Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi (TMA) na Wilaya pekee iliyowahi kutoa Mawaziri Wakuu ambao ni Edward Sokoine na Edward Lowassa.

Monduli. Waziri wa Kilimo, Godfrey Chongolo amewataka wananchi wa Jimbo la Monduli kudumisha amani ya nchi na kujivunia kuwa Wanamonduli kwa kuwa wilaya pekee iliyotoa mawaziri wakuu wawili.

Chongolo amewataja mawaziri wakuu hao ni Edward Sokoine na Edward Lowassa ambao wote wamekwisha kufariki dunia huku akigusia upekee wa Monduli ndani Jeshi la Ulinzi wa Wananchi Tanzania (JWTZ) kwamba ili askari apate nyota ya kwanza lazima apite Monduli.

Monduli ni miongoni mwa wilaya sita za Mkoa wa Arusha ambapo kuna Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi (TMA).

Chongolo ambaye amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapunduzi (CCM) amesema hayo jana Alhamisi, Julai 23, 2026 wakati akiweka jiwe la msingi la uzinduzi wa Kituo cha Afya Lowassa Sepeko, kilichopo Kijiji cha Mti Mmoja, Kata ya Sepeko wilayani Monduli.

“Nimefurahi kuja Monduli na hata mimi ningefurahi kuzaliwa Monduli. Hii wilaya ni ya muhimu kwelikweli, vijana wakakamavu ukiwaona wana mawe mawe (nyota mabegani) wamepita kwenye hii wilaya, huwezi kuwa na mawemawe kama hujaja kwenye hii wilaya au Jimbo hili,” alisema Chongolo

“Hapa tuna historia ya mawaziri wakuu wawili, Edward Sokoine aliyefanya mambo makubwa kwa nchi yetu na Edward Lowassa. Kwa historia ya jina hili, jina tu linatosha kutatua matatizo yetu, hata ukienda jeshini na kueleza tuna changamoto hizi na hizi wanakuja kutatua,” alisema.

Kuhusu maendeleo ya kituo hicho, Chongolo alisema atakwenda kusuma kwelikweli ili kupatikana fedha za kujenga jengo la X Ray ya kisasa: “Serikali kwa upendo mkubwa imeleta Sh200 milioni na kesho italeta tena. Kikubwa niwaombe sana tuilende hii nchi, hii nchi ndio farahi yetu na ndio ukombozi wetu.”

Kwa upande wake, aliyewahi kuwa Mbunge wa Monduli (CCM), Fredrick Lowassa yeye alitoa shukrani kwa Waziri Chongolo kwa kuzindua kituo hicho akisema safari ya ujenzi wa kituo hicho kilikuwa ndoto ya wakinamama wa Sepeko kwa miaka mingi  ambapo ujenzi ulianza Juni 23, 2023.

“Baada ya kuhamasisha wananchi, siku hiyo tukafanya harambee iliyotuwezesha kupata Sh248 milioni, mifuko ya saruji 1,100, nondo tani moja na tofali 6,000,” alisema Fredrick.

Fredrick amewapongeze wananchi na viongozi wa Kijiji cha MtiMmoja na wananchi wa Kata ya Sepeko kwa usimamizi bora kabisa wa ujenzi wa kituo hicho cha afya.

“Kituo hiki cha afya, alichokizindua Chongolo, hakitahudumia tu mamia ya wananchi wa Monduli na viunga vyake, bali pia wananchi watakaopata dharura wakiwa safarini kuelekea Makao Mkuu ya nchi Dodoma, Singida na kwingineko.

“Hata watalii wanaotembelea mbuga zetu za Manyara, Ngorongoro, Serengeti ambao wanapitia kwenye eneo hili lililopo barabara kuu kwenda na kutoka kwenye vivutio vyetu vya utalii,” amesema.

Fredrick ambaye ni mtoto wa kwanza wa Edward Lowassa alisema: “Pamoja na yote hayo, nimefurahi kwa Mheshimiwa (Chongolo) kutuacha na ujumbe mzuri wa sisi kujivunia kuwa wana Monduli, eneo alilosema hata yeye angetamani angezaliwa.”

Alisema anaamini maneno hayo yatazidi kuwafanya kutembea kifua mbele  wakizidi kujivunia na kuheshimu waasisi wa Wilaya ya Monduli waliofanya wilaya na jimbo hili lijulikane nchi nzima.

Naye Joseph Mesopiro, Mkazi wa Sepeko ameshukuru kuzinduliwa kwa kituo hicho na kupewa jina la Lowassa kwani:“Ni mbunge aliyefanya mambo makubwa kwenye elimu, licha tunamkumbuka Sokoine lakini Lowassa amewezesha sana shule za kata ndani na nje ya Monduli.

“Lengo ni kumuenzi na kuenzi maendeleo kwani tungeweza kuita jina lolote kama la Zahanati ya Samia au Kikwete lakini tumeamua kuiita jina la Lowassa ili kumuenzi Mzee wetu.”