Chongolo atembelea karakana ya Kipanya, atoa maagizo

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM,Daniel Chongolo ametoa siku Saba Kwa taasisi za serikali ikiwemo Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kukagua gari lake kama linakidhi viwango

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM, Daniel Chongolo ametoa siku Saba Kwa taasisi za serikali ikiwemo Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwenda kukagua gari iliyotengenezwa na Ali  Masoud "Kipanya".

Akizungumza leo Aprili 12, 2022 baada ya kutembelea karakana ya Kipanya iliyopo Vingunguti,amesema     taasisi hizo zinatakiwa kwenda  kujiridhisha na kutoa ushauri wa kitalamu gari na kama litakuwa limekidhi vigezo vyote walipatie alama ya ubora.

"Na walisajili kwenye alama ya ubora Ili tutoke hapo kwenda sehemu zingine lakini pia na taasisi zingingine kama Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), na zingine zote zinazohusika na wabunifu ndani ya siku Saba wafike hapa,"amesema Chongolo

Pia ameviomba vyuo vikuu ikiwemo cha Dar es Salaam kushiriki na kuhakikisha wanaboresha wazo hilo kwa kushirikiana na Masoud mwenyewe.

"Tunataka tufanye hivi Ili baadae tupate bidhaa nzuri zaidi na Shughuli zote nitaratibu mwenyewe na ndani ya siku 14 niwe nimefika mwenyewe hapa na timu yote, watoe majibu katika sehemu yao"amesema

Masoud ameshukuru Kiongozi huyo Kwa kutembelea kwenye karakana yake na kudai kwamba ujio wake utazidi kuitangaza bidhaa hiyo na kuwaaminisha wateja ni kitu bora.

"Katibu mkuu pamoja na nafasi yake kwa kazi aliazo nazo lakini ametenga muda kuja huku ni suala ambalo kwetu limetupa uzito na umetuongezea nguvu kwa kutotukatisha tamaa,"amesema

Gari hiyo inayotumia umeme ina uwezo wa kubeba kilo 500 ya mzigo, ilizinduliwa Aprili 2 mwaka huu. Ikichajiwa inatembea kilomita 60 na mzigo wakati bila mzigo ni kilomita 80.